Halmashauri ya wilaya ya Kilosa imeendelea kuneemeka na fedha mbalimbali toka Serikali Kuu katika kuwaletea maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, kwa uwepo wa ujenzi wa shule ya msingi Tambukareli katika kata ya Mikumi
Akizungumzia ujenzi wa shule ya hiyo ambayo imezinduliwa rasmi tarehe 06/03/2023 Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi na Awali Bi. Zakhia Fandey amesema ujenzi wa shule hiyo umetokana na fedha kutoka Serikali Kuu chini ya mradi wa GPE LANES II kwa shilingi milioni 400, ambapo shule ina vyumba vya madarasa 11.
Fandey amesema shule hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu, kuinua ari ya wanafunzi kupenda shule kutokana na uwepo wa mazingira bora ya ujifunzaji.
Akizungumzia faida na umuhimu wa uwepo wa shule hiyo Mratibu wa elimu kata ya Mikumi Yusta Ndelwa amesema kupitia uwepo wa shule hiyo umepunguza mrundikano wa idadi kubwa ya wanafunzi madarasani, lakini pia itaongeza usalama wa wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za msingi za Mikumi, Mikumi Mpya na Mikumi Town ambapo awali walikuwa wakivuka barabara lakini kwasasa watakuwa salama zaidi.
Aidha amesema wanaishkuru sana Serikali ya awamu ya sita kwa kuitazama Mikumi kwa jicho la tatu, kwani wamefanikiwa kupata madarasa na madawati ya kutosha sambamba na uwepo wa vyoo stahiki ambavyo pia vimezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ibrahim Chembe amesema kupitia fursa hiyo imewajengea wanafunzi na walimu mazingira na ari nzuri ya ufundishaji na ujifunzaji ambapo imeanza na wanafunzi 432 kuanzia elimu ya awali hadi darasa la sita na kwamba matarajio ni kuwa na wanafunzi 700 kwa shule nzima.
Sambamba na hayo wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Mikumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Mheshimiwa Diwani wa Mikumi ,viongozi wa kata pamoja na wananchi kwa juhudi mbalimbali walizozionyesha kuhakikisha uwepo wa shule hiyo kwa maslahi ya wanafunzi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa