Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Yohana Kasitila ametoa rai kwa waheshimiwa madiwani na watendaji wa kata kuwa mstari wa mbele kukemea mapungufu mbalimbali yanayojitokeza katika usimamizi wa miradi na rasilimali za umma kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia miradi na rasilimali hizo kutunzwa ipasavyo ili kuweza kufaa kwa matumizi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Rai hiyo imetolewa wakati wa kikao kilichoandaliwa na taasisi ya Dira Theatre kilichohusu mrejesho wa utekelezaji wa mradi wa wajibu wa jamii na viongozi katika kufuatilia na kusimamia matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya elimu ambapo amesema kuwa viongozi wanayo nafasi kubwa katika kuhamasisha jamii na kuhakikisha wananchi wanashiriki kwa kiwango kikubwa kutunza rasilimali hizo ambazo wao ndio wahusika wakuu kuona zinapatikana na zinatumika ipasavyo katika maeneo yao.
Kasilila amesema kuwa madiwani na watendaji wa kata wanao wajibu wa kuhakikisha mikutano na vikao vya kisheria vinafanyika ipasavyo kwani kupitia vikao hivyo vinavyohusisha wananchi vitatoa fursa kwa wananchi hao kujua kinachoendelea na ushiriki wao kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kwa kiasi kikubwa uwepo wa maendeleo kiujumla ikiwemo katika sekta ya elimu.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari waliohudhuria kikao hicho kuhusu kushuka kwa kiwango cha ufaulu wilayani Kilosa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mwambambale amesema kiwango cha ufaulu hakijashuka bali kimepanda kwani ufaulu umepanda kutoka 59% hadi 63% na kwamba licha ya ukubwa wa Wilaya na wingi wa shule, upungufu wa walimu, masuala ya mila na desturi na changamoto nyinginezo Halmashauri imejiwekea mipango madhubuti ya kuongeza kiwango cha ufaulu na elimu kwa ujumla na kwamba kwa sasa ofisi yake imepeleka ombi Ofisi ya Rais kuongeza nguvu katika umaliziaji wa majengo ya madarasa pamoja na kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa, viti na madawati.
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya Dira Theatre Erasmo Tullo amesema mradi huo unafanya kazi katika kata za Zombo, Masanze, Mabwerebwere, Mabula, Mbumi, Mtumbatu, Mkwatani, Lumbiji, Kilangali, Tindiga, Ulaya, Kasiki, Magomeni na Mamboya lengo ikiwa ni ufuatiliaji wa rasilimali za umma ni kuweka bayana matumizi sahihi ya rasilimali za umma, kuboresha hali ya utoaji huduma upande wa elimu na kukuza uwajibikaji jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na nidhamu ya matumizi ya rasilimali hizo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa