Watendaji wa kata wametakiwa kuhakikisha wanasimamia vyema suala zima la lishe katika maeneo yao ikiwemo kutunga sheria ndogo ndogo zinazoelekeza usimamizi wa makuzi na malezi muhimu kwa watoto lengo ikiwa ni kuhakikisha wilaya inakuwa na kizazi kilicho bora chenye kuzingatia hatua zote muhimu katika ukuaji wa mtoto toka anapokuwa tumboni hadi kuzaliwa sambamba na kuzingatia upatikanaji na matumizi ya lishe bora kwa mama mjamzito hadi mtoto chini ya umri wa miaka mitano.
Agizo hilo limetolewa Disemba 23 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati wa kikao cha kamati ya lishe na watendaji wa kata ambapo ametaka kila kata na kijiji kuwa na sheria ndogo ndogo ambazo zinapaswa kutekelezwa na jamii husika katika kuhakikisha malezi na makuzi ya mtoto yanazingatiwa ipasavyo kwa kuzingatia uhudhuriaji wa kliniki kwa mama mjamzito na suala zima la lishe ili kuepusha watoto kutokuwa na utapiamlo kwani lishe ndiyo inayojenga msingi wa ukuaji wa mtoto.
Mgoyi amesema endapo mtoto atakosa lishe bora itapelekea kupata utapiamlo lakini pia kuwa na ufaulu wa chini shuleni, hivyo kila mmoja kwa sehemu yake anao wajibu wa kushiriki kikamilifu kwa kushirikiana na wahudumu wa afya waliowezeshwa kutoa elimu ya lishe majumbani ili kuisaidia jamii kuzingatia upatikanaji na matumizi ya lishe bora jambo litakaloleta matokeo chanya kwa jamii huku akitaka suala la lishe kuwa ni ajenda muhimu katika vikao vya mabaraza ya maendeleo ya kata na vijiji ambapo amesisitiza kuwa endapo litazingatiwa itasaidia wilaya kiujumla kuwa na takwimu sahihi za lishe kwa kila kata na kijiji pia kila kijiji kinapaswa kuweka utaratibu wa kuadhimisha siku ya lishe kwa kila kijiji ambapo jamii itapata wasaa wa kupata elimi ya makuzi na malezi ya mtoto pamoja na lishe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amewataka watendaji hao kushirikiana kwa ukaribu na wahudumu wa afya wanaotoa elimu ya lishe majumbani kwa kuhakikisha wanatoa elimu hiyo ikwemo kusimamia matumizi ya baiskeli walizopewa kutotumika kwa matumizi binafsi badala yake zitumike kama ilivyokusudiwa kama chombo cha usafiri ili kuifikia jamii na kutoa elimu na kwamba kupitia ushiriki wao itasaidia kufanya ufuatiliaji jambo litakalosaidia kujua hali ya lishe kiuhalisia katika maeneo yao ya kiutawala.
Akifunga kikao hicho Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila amesema suala la lishe ni ajenda muhimu sana kwa watendaji wa kata kushiriki kikamilifu pia amewataka kutatua kero za wananchi kupitia vikao badala ya kusubiri kero hizo kufikishwa kwa Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi wakati kero hizo zinatakiwa zitatuliwe katika ngazi za vijiji na kata lakini pia wametakiwa kujipima utendaji wao wa kazi huku akisisitiza usimamizi wa usomaji wa taarifa za mapato na matumizi, kufanyika kwa vikao vya kisheria, usimamizi wa sheria mbalimbali na utekelezaji wake sambamba na kujiwekea mpango kazi wa majukumu yao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa