Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe S. Kebwe April 09 2018 amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kilosa na kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo inayoendelea wilayani Kilosa ikiwemo kutembelea baadhi ya mashamba ya pamba ili kujionea kinachoendelea baada ya kufanyika hamasa kwa wananchi miezi michache iliyopita ili walime pamba kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Katika ziara yake Mhe. Kebwe ametembelea mashamba yanayolimwa na viongozi wa wilaya, mashamba ya watumishi wa serikali pamoja na ya vikundi mbalimbali, ambapo amesema kuwa suala la soko halina mashaka kwani kampuni ya biosustain iko tayari kununua pamba yote itakayolimwa kwa bei nzuri na kwamba vinu kwa ajili ya uchambuzi wa pamba vipo hapa hapa mkoani Morogoro, jambo ambalo litasaidia upatikanaji wa ajira pamoja na kumpunguzia gharama mnunuzi wa pamba kwa kutosafirisha pamba na kuipeleka kuchambua eneo jingine.
Kwa niaba ya wakulima wenzao Njile Jibusa na Mipawa Masule wa kata ya Msowero wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa elimu ya kitaalam ya kilimo cha pamba kupitia maafisa ugani pamoja na kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo jambo ambalo limewapa hamasa kubwa kujikita katika kilimo cha pamba.
Kabla ya kutembelea mashamba hayo ziara hiyo ilitanguliwa na ukaguzi wa mradi wa barabara inayojengwa mjini Kilosa yenye urefu wa km 3.9 ambayo imebainika kuwa licha ya kutokamilika lakini pia imejengwa kwa kiwango cha chini, hivyo Mkuu wa Mkoa ameiagiza Takukuru Wilaya kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya kuhakikisha mkandarasi wa barabara hiyo anakamatwa ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa