Suala la utoaji lishe shuleni limeendelewa kusisitizwa katikati ya jamii kwa kila mmoja kushiriki kwa khakikisha inakuwa ni ajenda ya kudumu kwa lengo la kuimarisha na kujenga afya za wanafunz ili waweze kupata chakula pindi wawapo shuleni jambo litakalosaidia wanafunzi kupata elimu kwa kuzingatia masomo yao vizuri.
Msisitizo huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka H Shaka wakati wa kikao cha tathmini ya lishe kilichojumuisha mada mbalimbali ambapo amesema kuwa suala la lishe ni shirikishi kwa jamii nzima kwani upatikanaji wa chakula hutegemea na aina ya chakula kinachopatikana katika maeneo husika, hivyo si lazima chakula kiwe ni mahindi na maharage bali ukusanyaji wa vyakula uzingatie nyakati na upatikanaji wake katika maeneo husika.
Pamoja na hayo ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuweka mikakati ya uwepo wa sheria ndogo zitazoweka mkazo juu ya upatikanaji wa chakula mashuleni ambapo pia amesisitiza watendaji wa kata kushirikiana kwa ukaribu na jamii husika na uongozi wa vijiji kwa kuwa na vikao vya pamoja ili kupata suluhu ya upatikanaji wa chakula shuleni kwa watoto wote ikiwemo kutumia mbinu mbalimbali za ushawishi ili kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la upatikanaji wa chakula shuleni na kwamba kwa agizo hili kila mtendaji atapimwa namna anavyotekeleza agizo hili.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya(CCM) Comrade Shaban Mdoe ametaka Baraza la Maendeleo ya kata(BMK) kufanyika inavyotakiwa na kuifanya ajenda ya upatikanaji wa chakula kuwa ajenda muhimu na shirikishi ikiwemo upatikanaji wa maeneo ya kulima mashamba ya shule, upangaji wa bajeti ya chakula shuleni, huku upande wa ugonjwa wa kipindupindu ametaka kuendelea kutolewa kwa elimu ya afya na usafi wa mazingira inazingatiwa kwa kuzingatia matumizi ya maji safi, uimarishaji wa miundombinu ya maji na matumizi ya vyoo bora na salama.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mpella Kwidika ambaye mhasibu toka kitengo cha fedha amesema kuwa watendaji wa kata wamepewa dhamana ya kuongoza katika maeneo yao hivyo wanalo jukumu la kusimamia utekelezaji wa agizo la upatikanaji wa chakula mashuleni ni vema wakazingatia zaidi mazingira ya maeneo yao ili kuleta matokeo mazuri kwa kuzingatia zaidi matumizi ya njia shirikishi kwa jamii kwa jamii husika kushiriki kwa ukubwa zaidi kutoa mawazo yao kupitia mikutano ya vijiji na kamati za shule jambo litakaloleta tija kwa wanafunzi .
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Afya Dkt. Mameritha Basike amesema Divisheni ya Afya inaendelea kusimamia suala la lishe na utekelezaji wa agizo la Rais lakini pia inaendelea kutoa elimu ya usafi wa afya na mazingira katika maeneo mbalimbali huku akitoa rai kwa watendaji kuendelea kuhamasisha suala la usafi wa mazingira kwa wnanchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani na maeneo ya biashara ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa