Imeelezwa kuwa matokeo ya utafiti pekee hayawezi kuleta tija endapo wadau wengine hawatayachukua na kuyasambaza kwa watumiaji kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambavyo kwa asilimia kubwa vina uwezo wa kufikisha ujumbe kwa jamii husika ama walengwa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mh Omary Mgumba katika siku ya maonesho ya kilimo biashara ambapo amesema amezitaka taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania(TARI) na baraza la nafaka ukanda wa Afrika Mashariki(EAGC) kutambua kuwa vyombo vya habari vikitumika ipasavyo vina mchango mkubwa katika sekta ya kilimo kwani vitasaidia kuhamasisha matumizi ya teknolojia sahihi za kilimo kwa nia ya kuongeza tija.
Mgumba amesema kuwa kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na taifa hususan katika kuufikia uchumi wa kati ambao unategemea zaidi uwepo wa wakulima katika kuzalisha malighafi ambazo zitatumika viwandani na kuzalisha bidhaa mbalimbali zitakazokuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kiujumla.
Pamoja na hayo Mgumba amesema katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, upungufu wa rutuba ya udongo, visumbufu vya mazao na mengineyo taasisi za utafiti wa kilimo zimejielekeza katika kuongeza uzalishaji na uhamasishaji matumizi ya mbegu bora, kueneza elimu juu ya kanuni bora na endelevu za uzalishaji mazao ii kuongeza tija na faida, kueneza teknolojia rafiki kwa jinsisa zote katika uzalishaji na usindikaji mazao katika mnyororo wa thamani na kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi ili kueneza matokeo ya utafiti kwa walengwa kwa kasi katika maeneo husika.
Aidha ametoa wito kwa wananchi na wakulima kiujumla kutumia fursa hiyo kujifunza teknolojia mbalimbali ambazo zitawasaidia kuboresha kilimo katika maeneo yao ikiwemo kulima mazao yanayostawi maeneo yao kwa kuzingatia teknolojia zitakazowaletea tija.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amezitaka taasisi za utafiti hasa katika sekta ya kilimo kufanya shughuli za utafiti kwa karibu zaidi na wakulima ambao ndio watumiaji wakubwa wa matokeo ya tafiti hizo lakini pia ameiomba wizara ya kilimo kuwatupia jicho la karibu wakulima kwa kuwasaidia kupata maeneo ya kilimo ili kujiongezea kipato chao na taifa kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa