Kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wawezeshaji wa Halmashauri kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF na uhakiki wa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini wametakiwa kuzingatia misingi ya uadilifu katika kazi yao na kutotumia fursa hiyo kwa kutengeneza mazingira ya rushwa.
Rai hiyo imetolewa Julai 20 mwaka huu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wawezeshaji hao ambapo amewataka kuzingatia misingi ya uadilifu katika utendaji kazi kwa kutenda haki na kuzingatia misingi ya utumishi wa umma.
Mwambambale amesema katika eneo la uwajibikaji na uadilifu katika zoezi hilo la uhakiki ni vema kazi ikafanyika vizuri kwani kazi hiyo inahitaji umakini, weledi na upembuzi yakinifu ili kutoaji haki kwa kadri inavyostaki.
Naye Afisa Program wa TASAF Karim Kondo akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF amesema tathmini ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF inaonyesha mpango wa kunusuru kaya maskini nchini umechangia kwa kiasi kufikiwa azma ya Serikali ya kupunguza umaskini wa mahitaji ya msingi kwa kaya kwa 10% na umaskini uliokithiri umepungua kwa 12% kwa kaya maskini nchini.
Kondo amesema katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mfuko wa TASAF III kitatekelezwa katika Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar na kujumuisha maeneo ambayo hayakupata fursa katika kipindi cha kwanza cha utekelezaji ambacho kimekamilika mkazo mkubwa ukiwa katika kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango wa kufanya kazi ili kuongeza kipato.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Ufatiliaji TASAF Bi. Simth Haule amesema madhumuni ya Mpango katika kipindi cha pili ni kuwezesha kaya za walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato na huduma za jamii na uchumi na kuwekeza katika kuendeleza watoto wao huku msisitizo ukiwa katika kuwezesha kaya kufanya kazi ili kuongeza kipato, kuwezesha kaya kuongeza rasilimali zalishi na vitega uchumi, kuwekeza katika rasilimali watu hususan watoto ili kuleta matokeo chanya yatakayodumu kwa muda mrefu, kuboresha upatikanaji wa huduma za maji, afya na elimu pamoja na kukuza uchumi wa eneo unakofanyika utekelezaji kutokana na matokeo ya Mpango.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa