Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) tangu mwaka 2000 lengo likiwa ni kuongeza kipato, fursa na kuongeza uwezo wa kugharamia mahitaji mengine ya kaya za walengwa kupitia utekelezaji wa sehemu kuu nne za mpango huo.
Akieleza sehemu hizo za mpango huo wa TASAF Mei 08 2018 Afisa Mafunzo na Ushirikishwaji Catherine Kisanga wakati akitoa mafunzo kwa kwa waheshimiwa madiwani wa Wilaya ya Kilosa amesema kuwa sehemu hizo ni uhawilishaji fedha na ajira za muda, mpango wa kuweka akiba na kukuza uchumi, kuboresha miundombinu na kujenga uweza katika ngazi mbalimbali za utekelezaji.
Lengo la Mpango Kuweka Akiba ni kuongeza uwezo wa kuzalisha kipato cha kaya ili walengwa waweze kujisimamia wenyewe kwa vipindi vya kati na muda mrefu kwa kuwajengea uwezo wa uzalishaji hatua kwa hatua za kujitegemea kiuchumi kwa kaya na kuongeza vyanzo vya kipato,kwani unachangia ujenzi wa msingi wa kutoka kwenye umaskini kwa kuongeza uwezo wa kaya kujisimamia na kuimarisha kipato kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo,biashara na kazi za ujira.
Akieleza ni namna gani mpango huo utafanyika amesema walengwa watapata elimu kuhusu stadi za maisha usimamizi wa bajeti ya kaya pia watafahamishwa fusra za mpango, jinsi ya kupata huduma za ugani, kuzalisha kwa tija, jinsi ya kupata masoko na kuongeza thamani.
Sambamba na hayo walengwa watahamasishwa kujiunga kwenye vikundi vya akiba na kuwa malengo yenye tija huku wakipata maelezo na habari mbalimbali za mambo yanayokidhi mahitaji yao kama vile ruzuku za mitaji ili kukuza na kuendesha miradi ya kuzalisha kipato kwa kaya.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Hassan Mkopi kwa niaba ya madiwani wote licha ya kuishukuru TASAF kwa kuwajengea uelewa juu ya mpango huo, amewataka madiwani wenzake kushiriki kikamilifu katika kata zao kusimamia mpango huo kwa kuhakikisha walengwa wanafikiwa na kupata huduma stahiki hatimaye kuinuka kiuchumi na kufikia malengo ya millennia.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa