Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mwambambale ametoa rai kwa serikali za vijiji vya Tindiga A, Tindiga B na Ngaite kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea katika vijiji hivyo kwa njia ya suluhu kwa maslahi mapana ya wananchi wa vijiji hivyo na kwamba wakati wa migogoro umekwisha bali wakati uliopo ni kwa ajili ya kufanya maendeleo.
Mwambambale amesema kuwa wakati tuliopo ni wakati wa kutafuta maendeleo na kwamba mgogoro wa mipaka uliopo katika eneo la kwa kaburi la Madinda, kwa Kiduna na kibao cha Erato ni mgogoro unaoweza kutatuliwa kwa njia ya kukaa kwa pamoja kufanya suluhu kwani kuendelea kwa mgogoro huo kunaikosesha Halmashauri mapato ambayo ingeyapata kupitia wakulima na wafugaji.
Aidha Mwambambale ameiasa jamii ya wafugaji kutochukua sheria mkononi kwa kufanya maamuzi yasiyofaa na kusababisha migogoro na watambue kuwa hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria hivyo kila mmoja anapaswa kutii sheria ili tuweze kuishi kwa amani kwani wanakilosa wote ni jamii moja na ni ndugu na kwamba wanapaswa kuishi kwa ushirikiano huku kila mmoja akimhesabu mwenzake kuwa ni bora.
Sambamba na hayo katika kikao hicho iliundwa kamati ya pamoja yenye wajumbe 15 kutoka vijiji vyote vitatu itakayotambua ukubwa wa eneo lenye mgogoro, itatambua maeneo yaliyogawiwa kwa wananchi kwa ukubwa wake, itabainisha maeneo yanayolipiwa baada ya kugawiwa na kiasi cha fedha kilichopokelewa kwa maeneo hayo na kwamba kamati hiyo inaanza kazi mara moja wakati huo taratibu nyingine za kisheria zikiendelea ili kubaini umiliki halali wa eneo hilo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa