Wananchi wilayani Kilosa wametakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimbali wanaoonyesha nia ya kufanya kazi na wilaya ya Kilosa kwa lengo la kuleta maendeleo hususani katika shughuli za miradi mbalimbali ya maendeleo kwani miradi hiyo ni kwa faida ya wananchi na vizazi vyao.
Rai hiyo imetolewa Julai 16 mwaka huu na Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kilosa Reginald Samba aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Katibu Tawala Wilaya katika hafla ya makabidhiano ya majukumu ya uendeshaji mradi wa maji katika vijiji vya Mandela, Magole A na B vilivyopo katika kata ya Magole miradi ambayo imefadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali WARIDI ambalo linafadhiliwa na watu wa Marekani(USAID) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya kupitia ofisi ya RUWASA.
Simba amesema kuwa miradi huo wa WARIDI ni mradi unaoshughulika na kusaidia jamiii kupata maji safi na salama na kuboresha huduma ya maji ndani ya jamii ambapo kupitia miradi hiyo itapunguza kero ya maji kwa 90%, itaongeza makusanyo ya maji na kuendesha chombo cha watumia maji, kupata elimu ya ujasiriamali jambo litakalosaidia kukuza uchumi kwa wananchi lakini pia kuongezeka kwa shughuli mbalimbali zinazotumia maji ikiwemo ufyatuaji tofali, bustani ndogo ndogo na kukuza uchumi wa vijiji hivyo.
Pamoja na hayo Simba ameitaka RUWASA kuhakikisha inazifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizobainishwa na wananchi ikiwemo kuhakikisha wanafunga mita kwa wateja wa majumbani, kuhakikisha maeneo ambayo bado maji hayajafika yaweze kufikiwa, kujenga uelewa kwa wananchi namna ya utendaji kazi na utunzaji miundombinu ya maji lakini pia kuunda jumuiya ya watumia maji huku akitoa onyo kwa kwa wanajiunganishia maji kinyume cha taratibu.
Kwa upande wa gharama zilizotumika katika kutekeleza miradi hiyo ya maji kwa vijiji vya Mandela A na B ni shilingi 418,764,927.6 huku kijiji cha Mandela ukigharimu shilingi 379,875,068.26 ambapo katika makabidhiano hayo WARIDI imekabidhi michoro ya ujenzi pamoja na nyaraka zinazohitajika kwa Halmasharui na RUWASA.
Akieleza namna WARIDI inavyofanya kazi Mkuu wa Mradi Bigambo Nandiga amesema kwa asilimia kubwa WARIDI inafanya kazi na Mkoa wa Morogoro ambapo wamefanya shughuli mbalimbali katika maeneo mbalimbali ambapo katika Wilaya ya Kilosa licha ya miradi ya maji lakini pia imesaidia ujenzi wa vyoo katika shule tano zilizopo wilayani Kilosa lakini pia amesisitiza kuendelea kutunzwa kwa miradi hiyo kwa faida ya vizazi vijavyo ili idumu na kutoa matokeo tarajiwa.
Akizungumzia upatikanaji wa maji Meneja RUWASA Wilaya Injinia Josh Chum amesema RUWASA inatekeleza miradi ya maji maeneo mengi na kwamba hadi kufikia Disemba 2019 upatikanaji maji vijijini ilifikia 73% huku miji midogo ikiwa 85% na kwamba kwa kiwango kikubwa ukanda wa mikumi maeneo mengi yana maji ambapo kwa sasa kupitia ushirikiano wa WARIDI wapo katika ukanda wa tarafa ya Magole ambapo vinategemewa kuchimbwa visima 18 japokuwa ukanda huo una shida ya upatikanaji wa maji.
Aidha amesema zipo changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo usimamizi wa miradi, utekelezaji wa miradi kulingana na utaratibu unaotolewa na wadau ambapo pia amesema wamejipanga kuhakikisha maeneo yote ambayo hayana jumuia za watumia maji yanakuwa na jumuiya za watumia maji huku akiwashukuru wananchi kiujumla kwa ushirikiano walioutoa katika utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo kuchangia nguvu kazi katika miradi hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa