Shirika la reli Tanzania(TRC) linatarajia kufanya zoezi la uhamishaji makaburi yaliyopo katika maeneo yatakayopitia na reli mpya ya kisasa - Standard Gauge katika wilaya Kilosa katika kata za Mkwatani, Magomeni- Mkadage, Mabwerebwere-kijiji cha Kondoa, Chanzuru na Kimamba A – kijiji cha Kimamba.
Hayo yamebainishwa na mhandisi wa mradi wa reli mpya ya Standard Gauge Mhandisi Ismail A. Ismail katika kikao kilichohusisha viongozi wa idara za Ujenzi, Afya, Mazingira, viongozi wa dini na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo amesema zoezi hilo litahusisha vijiji vitakavyopitiwa na reli hiyo.
Ismail amesema kuwa lengo la zoezi hilo ni kuhakikisha linafanyika mapema kuhamisha makaburi hayo ili kupisha ujenzi wa reli hiyo sambamba na kuondoa vikwazo pamoja na ucheleweshaji kwa mkandarasi ili aweze kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za ujenzi wa reli ikiwemo kutokuwepo kwa vikwazo vya aina yoyote ile.
Tathmini ya utambuzi wa makaburi hayo umeshafanyika na makaburi 339 yanatarajiwa kuhamishwa ambapo tarehe 9/02/2019 kutakuwa na ziara ya kutembelea makaburi hayo pamoja na kutambua maeneo yatapohamishiwa makaburi hayo.
Ismail amesema kuwa zoezi kamili la uhamishaji litafanyika kuanzia mwezi huu wa pili kabla ya mvua kuanza na kwamba uhamishaji wa makaburi hayo utafanyika kwa gharama za Shirika la Reli nchini na kuwa makaburi yatakayohamishwa kutakuwa na kifuta machozi kwa ndugu husika.
Aidha ameongeza kuwa zoezi la uhamishaji makaburi hayo utahusisha Shirika la Reli Tanzania, wataalam wa Afya, Mazingira toka ofisi ya Mkurugenzi, Watendaji wa kata husika, kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa dini na jamii husika katika maeneo hayo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa