Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa John Kasitila ametoa rai kwa wasanii waliopo wilayani Kilosa kutumia vema fursa ya wao kuwa wasanii hasa katika ngazi ya utalii kwa kuiweka sanaa vizuri katika maeneo ya utalii ili watalii wa ndani na nje wanapotembelea maeneo mbalimbali ya kitalii wataweza kukuza uchumi ikiwemo kununua bidhaa zitokanazo na sanaa wanazozifanya kwa kutambua kuwa katika maeneo ya utalii si vivutio kama wanyama vinavyopatikana katika maeneo hayo lakini pia kazi za wasanii ikiwemo uchoraji, uchongaji vinyago, ngoma, miziki na sanaaa nyinginezo.
Rai hiyo imetolewa wakati wa kikao cha Katibu Tawala huyo kwa wasanii wa aina zote wilayani kilosa ambapo amesema kuwa iwapo wasanii hao wakijipanga vema na kujisajili katika Baraza la Sanaa Tanzania- BASATA itawasaidia kutambulika na kupata kibali cha kufanya kazi zao maeneo mbalimbali kwa uwazi jambo litakalowasaidia kupata misaada na utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
Katika kikao hicho wasanii hao wamesema ipo haja ya kuwa na mikakakti ya kufufua na kuendeleza sanaa ikiwemo kuanzisha mashindano ya sanaa na kujenga misingi bora ya sanaa kuanzia mashuleni, kuhakikisha kila msanii ama kikundi kinasajiliwa kisheria, itolewe elimu juu ya haki zao, lakini pia wajengewe misingi mizuri ya usimamizi na masoko ya kazi zao ili waweze kujikwamua kiuchumi, pamoja na kuwa na matamasha /makongamano yatakayowakutanisha kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu.
Naye mmiliki wa Kilosa club Deo Mwakabanga ametoa wito kwa wasanii hao kutumia fursa ya uwepo wa kumbi mbalimbali kuonyesha sanaa ama kazi wanazozifanya kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kutambulika lakini pia kujiongezea kipato kupitia kazi zao.
Naye Mwishehe Mohamed ambaye ni msanii ametoa wito kwa wasanii wenzake kutokuwa wavivu wa kutafuta habari ili kujua kila kinachojiri katika sekta ya sanaa kwani kwa kufanya hivyo itawaongezea uelewa wa mambo mbalimbali hususani ya sanaa na kuongeza juhudi ili kufikia viwango vya juu na kuikuza sanaa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa