Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa halmashauri 9 za Mkoa wa Morogoro zinazotekeleza mpango wa kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu lengo ikiwa ni kuondoa tatizo la wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi bila kuweza kumudu stadi hizo muhimu ambapo mpango huo unafadhiliwa na USAID Tusome pamoja kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Taznania chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Rais(TAMISEMI).
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati wa hafla fupi ya ugawaji wa pikipiki 40 kwa Waratibu Elimu Kata pamoja na ugawaji wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 24.5 kwa vikundi saba vya vijana na kinamama kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kupitia 4% ya vijana na 4% kwa kinamama ikiwemo pikipiki 6, mashine ya kufyatulia tofali, ,compresa, pump ya umwagiliaji na mashine ya kusaga na kukoboa.
Akitoa nasaha zake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema kuwa pikipiki hizo zimetolewa ili kuwawezesha na kuwarahisishia waratibu hao ufatiliaji kwa kila shule, hivyo wahakikishe wanazitunza na zinakuwa salama ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na zitumike katika makusudi yaliyokusudiwa na yoyote atakayebainika kuzitumia kinyume na makusudi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha kwa upande wa vikundi vilivyopokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya amewataka wanavikundi hao kuvitumia vifaa hivyo kwa ajili ya kuzalisha na kuchangia maendeleo kwani watakapozalisha itawasaidia kuinuka kiuchumi na kujiajri wao wenyewe.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilosa Mhe. Hassan Kambenga amewataka Waratibu Elimu Kata pamoja na wanavikundi hao kuhakikisha wanavitumia vifaa hivyo kwa umakini na kwamba wao kama viongozi hawatasita kufatilia mwenendo wa matumizi ya vifaa hivyo na kwa upande wa elimu amewataka waratibu hao kushirikiana na walimu walio chini yao ili kuhakikisha kiwango cha wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu inapungua na hatimaye kutoweka kabisa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa