Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewaasa wavuna miti, mkaa na kuni wilayani Kilosa kutumia kiuhalali vibali wanavyopata pasipo kufanya udanganyifu katika uvunaji wa mazao husika ili kutopoteza pato la taifa kwa kuvuna kinyume na maombi ya vibali hivyo yanavyoonyesha na kwamba atakayebainika kukiuka makubaliano hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mgoyi amesema hayo katika kikao kilichoshirikisha wavunaji wa mbao, kuni, mkaa, watendaji wa vijiji pamoja na wenyeviji wa vijiji ambapo amesema kuwa wapo baadhi ya wavunaji wamekuwa na hulka ya kuvuna mbao, mkaa ama kuni kwa kiasi kikubwa na kulipa kidogo ama kutoa taarifa za kutovuna huku uhalisia ukiwa wamevuna hivyo kusababisha mapato ya taifa na halmashauri kupotea kwa njia za udanganyifu kwa watu jambo linaloashiria kukosa uzalendo kwa nchi yao.
Sambamba na hayo katika kikao hicho yamefanyika makubaliano ya malipo ya leseni kwa ajili ya uvunaji kwa kila eneo ambalo mvunaji atakuwa ameliomba ambalo atapaswa kulipa 20% kabla ya kuanza kuvuna ili kuiingizia serikali mapato.
Naye Afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa amesema kuwa serikali za vijiji zinapaswa kujiridhisha kabla ya kutoa maeneo yanayoombwa na wavunaji ili kuepuka migogoro baina ya wavunaji kwa wavunaji kuwa eneo moja ambalo linaweza kupelekea uchache wa bidhaa na hatimaye wavunaji kujikuta wakivuna miti ambayo ni nje ya vibali walivyoomba.
Aidha taarifa ya uvunaji wa mazao ya misitu wilaya kwa mwaka 2017/2018 imeonyesha zao la magogo limevunwa kwa meta za ujazo 209, zao la mkaa meta za ujazo 4091 huku zao la kuni likivunwa kwa meta za ujazo 580.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa