Imeelezwa kuwa viongozi wa dini na siasa wanayo nafasi kuwa ya kuhamasisha jamii kuhakikisha kina mama wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma badala ya kuendelea kujifungulia kwa wakunga wa jadi au majumbani lengo ikiwa ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano pamoja na kuiimarisha jamii kuwa na afya bora ya uzazi na mtoto.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati wa kikao kilichohusisha viongozi wa dini na siasa ambapo amesema kuwa viongozi hao wano wajibu kuelimisha walio chini yao hasa wanaume kuthamini afya za wenza wao kwani serikali kwa upande wake inajitahidi kuhakikisha huduma husika zinapatikana hivyo viongozi wa dini na siasa licha ya kuongea masuala ya kidini lakini pia watumie majukwaa yao kuzungumzia elimu ya afya uzazi na mtoto.
Naye Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Wilaya ya Kilosa Sophia Mpunga amesema kuwa kitengo cha huduma za afya ya uzazi na mtoto kinatoa huduma ya upimaji wa wajawazito na maendeleo ya ukuaji wa mimba ambapo licha ya huduma hizo wamekuwa wakikumbana na changamoto zinazosababisha vifo kwa mama na mtoto ikiwemo kuchelewa kuanza kliniki, mahudhurio hafifu ya wenza wakati wa kuanza kliniki, uelewa mdogo kwa jamii kuhusu huduma za afya ya uzazi na mtoto hasa uzazi wa mpango na tatizo la kujifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi.
Aidha kikao hicho kilipata fursa ya kujadiliana namna ya kuweka mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka watu 16 hadi kufikia 10 kwa mwaka ambapo Mhe. Daud Mfaume diwani wa kata ya Kasiki na Mhe Yahaya Mwinchea diwani wa kata ya Mkwatani wametoa rai kuendelea kuhamasisha jamii kutumia njia salama za uzazi na kuzuia vifo pamoja na kupata takwimu sahihi ili kupunguza vifo na kushauri watu waende hospitali na wanaume kuacha kauli zisizofaa pindi inapohitajika kwenda kiliniki na wenza wao.
Nao viongozi wa dini kwa pamoja wameahidi kutumia misikiti na makanisa kuelezea waumini wao juu ya uzazi na kuachana na tabia za usiri lakini pia wametoa wito kwa wahudumu wa afya kuwa na kauli nzuri na upendo wanapopokea wagonjwa hali ambayo inatawahamasisha kina mama kujifungulia vituo vya kutolea huduma badala ya kukimbilia kwa wakunga wa jadi.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Tumaini Geugeu kwa niaba ya Mganga Mkuu Wilaya amesema licha ya sababu mbalimbali zinazosababisha vifo kwa mama na mtoto mimba za utotoni na ndoa ambazo sio rasmi ni miongoni mwa vyanzo vya vifo hivyo kwani zina madhara meengi ikiwemo ukatili, kubakwa, usiri katika kutoa elimu kwa watoto ili waweze kujitambua na kutokomeza mimba za utotoni.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa