Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh William Lukuvi ameitaka jamii na wananchi kwa ujumla kutambua kuwa lengo la kufuta mashamba ambayo serikali imekuwa ikiendelea kuyafuta ni kutoendelezwa na wanaoyamiki hali ambayo inasababisha wananchi kukosa mashamba ya kulima kwa ajili ya kujikimu kimaisha na kujiongezea kipato.
Lukuvi amesema hayo Mei 16 katika ziara yake wilayani Kilosa na kusema kuwa lengo la ziara yake ni kuitambulisha rasmi timu ya uhakiki wa mashamba yaliyofutwa ambapo timu hiyo itafanya upya uhakiki upya wa mashamba yote yaliyofutwa, historia ya mashamba hayo lengo ikiwa ni kupata uhalali wa wamiliki wa maeneo hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya mgawanyo kwa kuangalia wananchi wote wenye uhitaji ili kufanya uhalali ambapo ardhi nyingine itatengwa kwa ajili ya uwekezaji ili kutengeneza mazingira ya uwekezaji na upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro.
Aidha amesema kuwa wote walioko katika maeneo hayo wanapaswa kutambua kwa sasa si wamiliki wa maeneo hayo hadi hapo uhalali utakapofanyika ambapo zoezi hilo la kupata uhalali litafanyika kupitia timu hiyo yenye vifaa vya kutosha kutoka wizarani na kuhusisha uongozi wa wilaya na wananchi ambapo baada ya uhakiki na mapendekezo utafanyika mchakato wa ugawaji wa mashamba hayo utakaofanyika chini ya Wizara ya Ardhi na kwamba kila anyemiliki mashamba hayo atambue kuwa kuanzia sasa si wamiliki hadi hapo uhakiki na ugawaji utakapofanyika upya.
Sambamba na hayo amewataka wananchi wa maeneo yote yaliyo na mashamba yaliyofutwa kutoa ushirikiano na kuachana na hulka ya kugomea uhakiki unapofanyika kwani kitendo cha kugomea timu hiyo kutapelekea kukosa haki yao ya umiliki na kwamba timu hiyo haitosita kuendelea na kazi iliyokusudiwa lengo ikiwa ni kutoa uhalali wa ardhi ili kila anayepaswa kumiliki aweze kumiliki kiuhalali na kuepusha migogoro ama kuitwa wavamizi.
Naye Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Wilaya Ibrahim Ndembo ameushukuru uongozi wa Serikali ya awamu ya tano kwa juhudi wanazofanya katika kufuta mashamba yasiyoendelezwa ambapo hadi sasa jumla ya mashamba pori 25 yenye ukubwa wa ekari 23,596 yamebatilishwa katika maeneo ya Msowero Mvumi na Chanzuru ambapo mashamba 15 kati ya 25 yakiwa yamebatilishwa katika kipindi cha uongozi wa awamu ya tano baada ya wamiliki wake kushindwa kuyaendeleza sambamba na mashamba pori 8 yenye ekari 3816 kwa maeneo ya Magole na Masanze taarifa zake zimewasilishwa kwa kamishna wa ardhi kwa ajili ya hatua za ubatilishwaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa