Mkuu wa wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo fursa za ajira, kimaendeleo na kibiashara zitakazojitokeza kupitia ujio wa mradi wa reli ya kati na reli ya mwendo kasi (standard gauge) kwa kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na wilaya kiujumla.
Mgoi amesema kuwa ujio wa miradi hiyo miwili ni lulu kwani itatoa mwanya mkubwa wa maendeleo kwani kupitia reli hizo kutakuwa fursa kubwa za kutanuka kiuchumi ambapo wananchi watapata ajira, uchumi utapanda viwango na pia wawekezaji watawekeza katika maeneo mbalimbali yaliyopo wilayani Kilosa.
Akieleza kuhusu miradi hiyo Injinia Mlemba Singo ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati amesema mradi huo unalenga kukarabati reli iliyopo kwa kipande cha Dare s salaam – Isaka kwa Kilomita 970 ili kuinua uwezo wa kubeba mizigo toka tani 13.5 hadi tani 18.5 huku ujenzi wa reli ya kisasa amesema ni reli ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nguvu ya umeme yenye mwendo kasi usiopungua kilomita 160 kwa saa.
Singo amesema miradi hiyo italeta tija kwa wananchi kwani kutakuwa na ongezeko la usafirishaji wa mizigo ambapo reli itabeba mizigo mpaka tani 10000 kwa mkupuo, uokoaji wa muda wa kusafiri kwa abiria na mizigo, ongezeko la ajira , uboreshaji huduma za kijamii, kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, na faida za kiuchumi kwenye sekta ya usafirishaji hasa kupunguza gharama za mara kwa mara za matengenezo ya barabara.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa