Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilayani ya Kilosa Mhe. Hassan Mkopi ametoa rai kwa wanachama wa shirika lisilo la kiserikali – Campaign For Female Education(CAMFED) kujiunda katika vikundi na kujisajili ili kundi linalojulikana kisheria jambo litakalowasaidia kufaidika na fursa mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo mikopo na mitaji kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Mkopi amesema hayo Oktoba 26 mwaka huu wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mitaji mbalimbali kwa wanachama hao walio chini ya CAMFED na kusema kuwa mitaji hiyo ikatumike kama ilivyokusudiwa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kutumia vyema elimu waliyonayo ikiwemo kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Aidha amesema kuwa mitaji hiyo inahitajika kukua na yeye kama Mwenyekiti kwa kushirikiana na madiwani wenzake watafanya ufatiliaji kuona namna wanavyojiendesha huku akisisitiza wanachama hao kutokuwa waoga kuwatumia wataalam mbalimbali katika kukuza mitaji yao ikiwemo benki ya NMB pamoja na wataalam toka idara ya maendeleo ya jamii pamoja na idara nyinginezo.
Akisoma risala ya wanachama wa CAMFED Katibu wa mtandao wa Camfed Members Association(CAMA) Kilosa na Kitaifa Bi. Mzizi Mtambua amesema shirika hilo lenye lengo la kuwasaidia watoto wa kike walio katika mazingira hatarishi ili waweze kujikwamua kielimu pia kuondokana na umaskini mpaka sasa linafadhili shule za sekondari 28 na shule za msingi 54.
Aidha amesema kuwa shirika hilo linajivunia wasichana 1226 waliowahi fadhiliwa na CAMFED ambao wanajihusisha na shughuli mbalimbali ikiwemo ujasiliamali, kilimo, kujitolea kufundisha stadi za maisha katika shule za sekondari n.k
Katika hafla hiyo ya ugawaji mitaji hiyo kwa wanacama 2000 vimekabidhiwa vifaa, vitendea kazi pamoja na bidhaa za kuuza vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 84 ili kuwanufaisha katika miradi mbalimbali ambayo itasimamiwa na wataalam wote wa Halmashauri kiujumla , kamati ya CAMFED Wilaya watendaji wa vijiji na kata pamoja na waratibu wa CAMFED ili kuongeza nguvu katika miradi watakayoifanya ili wafikie malengo waliojiwekea.
Sambamba na hayo Mwenyekiti wa halmashauri ameuagiza uongozi wa Halmashauri kuandaa barua itakayoonyesha kuthamini mchango wa CAMFED kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa kusomesha wanafunzi mbambali kwa gharama kubwa kazi ambayo ilipaswa ifanywe na Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa