Rai imetolewa kwa wadau wote wilayani Kilosa kuunga mkono jitihada za serikali na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) pamoja na taasisi mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, salama na yakutosha ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda kwa kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi pasipo kusahau usimamizi mzuri wa miradi ya maji.
Rai hiyo imetolewa Oktoba 30 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe. S. Kebwe katika hafla ya uzinduzi wa miradi ya maji iliyotekelezwa na jamii kwa kushirikiana na mradi wa WARIDI katika kijiji cha Msowero kata ya Msowero wilayani Kilosa amesema kuwa mradi unalenga kuboresha upatikanaji wa maji kwa kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali maji kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho pia unalenga dira ya maendeleo ya taifa ili kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji na kuhakikisha kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama ifikapo 2025.
Mgoyi amesema kuwa maji ni muhimu katika maisha yetu kwani kumekuwa na matukio ya magonjwa ya kipindupindu hali ambayo imekuwa ikichangiwa kwa kukosa maji safi, salama na ya uhakika, hivyo mradi huo ni mkombozi hasa kwa kinamama kwa shughuli za kila siku ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa zikiathiriwa na ukosefu wa maji, hivyo uwepo wa mradi huo utapunguza tatizo la ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama ikiwemo kuwapunguzia mzigo mkubwa kinamama wa kutafuta maji.
Akisoma taarifa fupi ya mradi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Asajile Mwambambale Injinia Josh Chum amesema mradi huo ulikuja na sera ya kuwa na vyoo bora kwanza ambapo kwa hamasa ya wananchi waliweza kuchangia rasilimali fedha pamoja na nguvu kazi ambapo kiujumla mradi umegharimu shilingi milioni 469,237,660/= na kwa kupitia mradi wa WARIDI wananchi wamepunguza matatizo ya maji kwa 85%, kukuza uchumi kwa kutopoteza muda mwingi kutafuta maji safi, kuongeza kipato kwa kulima mbogamboga na ufugaji kuku kwa kutumia maji kidogo na kuongeza kipato cha kijiji kupitia mfuko wa maji kwa kuchangia huduma za maji.
Aidha Josh amesema kijiji cha Msowero kwa kushirikiana na mradi wa WARIDI, kampuni ya Water Pay na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wanakusudia kufunga mita za maji za kabla ya malipo katika vituo 26 vya kuchotea maji vya kijamii lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi wa kutoa maji kwa jamii na kuongeza mapato ambapo ufungaji huo wa mita upo katika hatua za uhamasishaji na mafunzo kwa jumuia ya watumia maji kuhusu namna ya kutumia mfumo huo kabla ya kufungwa mita hizo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa