Imeelezwa kuwa hali ya upatikanaji wa dawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imekuwa ya kuridhisha jambo linaloonyesha juhudi kubwa za kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa awamu ya Tano ikiwa ni sehemu ya ahadi zake kuwa atahahakikisha upatikanaji wa dawa unakuwa wa kuridhisha ikiwa ni ishara ya kuonyesha matokeo halisi ya fedha zinavyotumika.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Dkt. Ummy Mwalimu ambapo amesema kwa kuwa upatikanaji wa dawa ni mzuri hivyo amewasisitiza madaktari kuhakikisha utoaji wa dawa kwa wagonjwa unazingatia mwongozo wa taifa wa matibabu ambapo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Katibu Tawala Wilaya kuendelea kuwasisitiza madaktari kuzingatia mwongozo wa ugawaji dawa ka kadri unavyosema badala ya kugawa dawa kwa matakwa yao au ya mgonjwa.
Akizungumzia upatikanaji wa dawa pamoja na upatikanaji wa huduma za matibabu mwalimu amewataka maafisa maendeleo ya jamii kuwahamasisha wananchi kukata bima ya afya iliyoboreshwa ili waweze kupata huduma stahiki ikiwemo kupata dawa bila ya kukutana na kikwazo cha kifedha na kwamba mwananchi aliye na bima ya afya atapata huduma zote bure katika zahanati,vituo vya afya na hospitali.
Aidha mwalimu amesisistiza kujengwa kwa jengo jipya la wagonjwa wa nje(OPD) kwani lililopo sasa ni chakavu na halina mazingira ya kuridhisha ya utoaji huduma na kwamba ameishauri ofisi ya mkurugenzi kupanga kuwa na hospitali nyingine lengo ikiwa ni kusogeza huduma kwa wananchi na kwamba kwa upande wa serikali itajenga miundombinu ya afya kulingana na mazingira hapa nchini na kusisitiza upatikanaji na utoaji wa chanjo mbalimbali kwa wananchi hasa watoto chini ya miaka mitano kwani mahitaji ya chanjo ni makubwa.
Sambamba na hayo amesisitiza kuzingatiwa kwa afya ya mama na mtoto kwa kupunguza idadi ya vifo vya watoto na vifo vitokanavyo na uzazi kwani teknolojia ipo pamoja na vifaa kwani wanawake wengi wanachelewa kuanza kliniki, hivyo ni vyema kinamama wanapojiona wana dalili za ujauzito kuanza kliniki mapema jambo litakalosaidia kupata huduma stahiki ili kulinda afya ya mama na mtoto ili wawe salama.
Licha ya kutoa maelekezo na mambo ya kuzingatia Mwalimu ametoa pongezi kiujumla kwa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali ya Wilaya huku akisisitiza ujenzi wa vyoo bora kwa kaya ambao hazina vyoo bora na kuzingatia utoaji wa elimu ya kinga na kusisitiza lishe bora kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa