Licha ya mtoto kuonyesha juhudi zake za kutaka matokeo mazuri katika elimu yake mwalimu na mzazi wanao mchango mkubwa katika kuhakikisha malengo hayo chanya yanafanikiwa kwa mwalimu kuhakikisha anafundisha mada stahiki na kufanya ufatiliaji wa kina kwa kushirikiana na mzazi pamoja na mtoto husika.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati wa ziara yake ya siku mbili tarehe 4-5/09/2019 katika ukaguzi wa kambi za kidato za nne zinazoendelea katika shule mbalimbali za sekondari ambapo amesema kuwa hakuna mtoto ambaye hana akili isipokuwa kutofaulu kwa watoto kunatokana na ukosefu wa ushirikiano wa watu watatu ambao ni mwalimu, mwanafunzi na mzazi kwani usimamizi wa kutosha ukifanyika matokeo chanya lazima yatokee ambayo ni ufaulu mzuri kwa wanafunzi.
Aidha katika ziara yake hiyo aliyotembelea ujenzi wa kituo cha afya Malolo, zahanati ya Ruaha na Darajani na ujenzi wa chumba cha radasa shule ya msingi Ruaha Darajani pamoja na shule za sekondari Mikumi, Iwemba na Vidunda amewataka walimu na wakuu wa shule zote kufanya kazi kama timu kwa kufatilia ufundishaji wa kila mmoja kwa lengo la kusaidiana huku akiwasisitiza kuchukua matokeo ya mitihani na majaribio ya watoto kama kipimo cha ufundishaji wao jambo litakalosaidia kujua wapi pa kurekebisha ili kufikia malengo ya wilaya ya kuondoa daraja la nne na sifuri katika mitihani ya kitaifa kwa kidato cha pili na cha nne.
Pamoja na hayo amewataka viongozi wa kata zote kushirikiana na walimu kuwasisitiza na kuhakikisha wazazi wanafika shuleni nyakati za kuchukua ripoti za matokeo ya watoto wao ili kuwa na muda wa kukaa na walimu kujadiliana maendeleo ya watoto wao na kutatua changamoto za kitaaluma zinazowakabili jambo litakalosaidia kuongeza kasi ya ufatiliaji na kumsaidia mtoto.
Sambamba na hayo katika kukabiliana na suala la nishati ya umeme wakati wa usiku kwa ajili ya kambi zilizoko mashuleni Mgoyi ametoa taa za sola kwa shule ya sekondari Vidunda huku diwani wa kata ya Kidodi Mhe. Abdullatif Kaid akiahidi kuweka umeme katika madarasa yasiyopungua matano katika shule ya sekondari Iwemba.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa