Watendaji wa kata na vijiji wamekumbushwa kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma ambao ni viongozi katika maeneo yao hivyo wanapaswa kuwa mfano bora lakini pia wamekumbushwa kutambua kuwa ni wasimamizi wa shughuli zote katika maeneo wanayoyasimamia.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba ambapo amesema athari za usimamizi mbovu ni chanzo cha migogoro mbalimbali ambapo baadhi ya watendaji wamekuwa chachu ya migogoro kwa kutozingatia sheria, taratibu na kanuni..
Akionyesha kusikitishwa kwake na usimamizi mbovu ametoa agizo kwa watendaji wote ambao hawajasimamia vema suala la wanafunzi wa sekondari kutoripoti shuleni kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni ifikapo tarehe 14/02/2022 huku akisema kumekuwa na ukiukwaji wa maelekezo katika usimamizi wa mapato ambapo ametaka fedha zote zinazokusanywa ziingizwe katika akaunti kwaajili ya kufanya maendeleo ili kutowavunja moyo wananchi katika kuchangia maendeleo.
Kisena amesema ipo changamoto kubwa katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kupitia utoroshwaji wa mifugo na mazao, ukusanyaji feki wa ushuru, ukusanyaji kodi na mapato mengineyo ambapo kumekuwa na ufatiliaji na usimamizi mbovu ambao ni matokeo ya usimamizi mbovu wa mapato.
Aidha ametoa agizo kwa watendaji wote wenye mawakala waliopewa POS kufikia Jumatatu ya tarehe 14/02/2022 mawakala wote waliopo wote wawe wamebadilishwa sambamba na kubadilisha nywila(password) zote katika mashine za POS, huku akiwaagiza watendaji wa kata kuleta takwimu za maduka yote yaliyopo katika maeneo yao na kuziwasilisha ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji
Naye Mkuu wa Takukuru Wilaya Gwakisa Mwaipyana amewataka watendaji hao kujitathmini na kutimiza majukumu yao ili kuondoa malalamiko kwa wananchi pamoja na kutojihusisha na ukusanyaji fedha usio halali kwani ni kosa kisheria huku Mkuu wa Polisi Wilaya Venance Mapala akisisitiza utendaji kazi wenye weledi ikiwemo kuzingatia utoaji wa barua za dhamana kwa eneo husika na si vinginevyo sambamba na ufanyaji wa tathmini kwa wakati pindi migogoro inapojitokeza.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa