Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Kisena Mabuba ameishukuru Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Uongozi wa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kilosa fedha kwaajili ya Utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo katika Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo na Mifugo, miundombinu pamoja na maji na kusema kuwa fedha hizo zimeleta tija na kuchochea maendeleo kwa wana Kilosa.
Mkurugenzi huyo ametoa shukrani hizo kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa 02 Novemba 2023 wakati wa kikao na waandishi wa habari katika kampeni ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kushirikisha wadau mbalimbali wa Habari na wakurugenzi 9 kutoka Mkoa wa Morogoro.
Mabuba amesema kuwa katika sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu halmashauri imepokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi 5,565,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 5, Zahanati 18, ikiwemo Majengo ya X-ray , Wodi za mama na mtoto, nyumba za watumishi 3 pamoja na kiasi cha shilingi 1,350,000,000 kimepokelewa kwa ajili ya vifaa tiba vinavyotumika katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma kwani hapo awali wananchi walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kupata huduma hizo.
Sambamba na hayo amesema kuwa katika Sekta ya Elimu Halmashuri imepokea kiasi cha shilingi 2,046,000,000 kutoka serikali kuu kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa shule 6 za awali na msingi pamoja na kiasi cha shilingi milioni 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 4 , Katika Mradi wa SEQUIP halmashauri imepokea kiasi cha fedha shilingi 2,526,995,275 kwa ajili ya ujenzi wa Shule 5 za Sekondari ikiwemo na kiasi cha shilingi 190,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 4, Hivyo kurahisisha mazingira ya kusomea na kufundishia kwa wanafunzi.
Aidha Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kwa sasa adha ya kutembea umbali mrefu ili kufika shuleni na Mrundikano wa Wanafunzi katika madarasa umepungua hali iliyochochea wananchi kujitokeza kwa wingi katika kuandikisha watoto kujiunga na Elimu ya awali na Msingi, huku utoro wa wanafunzi ukipungua kwa kiasi kikubwa
Mabuba ameongeza kwa kusema kwa kipindi cha miaka mitatu Vikundi mbalimbali vimepokea mkopo jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 1,205,924,367.84 kwa ajili ya kufanya shughuli za kimaendeleo ili waweze kujikwamua kiuchumi, Mikopo ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, na kusema kuwa vikundi hivyo ni kama vikundi vya wanawake 41, Vijana 31 na watu wenye ulemavu 31.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa