Katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kwa Kipindi cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Disemba kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika 27 Februari, 2025 hoja ya uvamizi wa tembo katika mashamba ya wakulima wa Kata ya Mhenda imeibuliwa na kutolewa mapendekezo.
Akitoa hoja hiyo katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Mhenda Mhe. Japhet Nestory Kageuka, amesema kuwa Tembo wamesababisha madhara makubwa kwa wakulima, ambapo jumla ya hekari 80 za mashamba zimeharibiwa na wakulima 23 wameharibiwa mazao ya biashara na chakula.
Mhe. Kageuka ameongeza kuwa uvamizi wa tembo katika vijiji vilivyozunguka kata hiyo umeleta hasara kubwa kwa wakulima na kwamba hali hiyo imeleta changamoto kubwa kwa wakulima ambao sasa wanakosa tija kutokana na uharibifu wa mazao yao ambapo inahitajika kuangaliwa kwa makini ili kupunguza athari kwa wananchi.
Aidha Diwani Kageuka ametoa mapendekezo kwa serikali ya wilaya ya Kilosa kuhusu namna ya kukabiliana na tatizo hilo ambapo ameiomba serikali kutuma wataalamu wa wanyamapori ili kutoa elimu kwa wakulima kuhusu jinsi ya kulinda mashamba yao kutokana na uvamizi wa tembo huku akisisitiza umuhimu wa kuwapa mafunzo vijana wa eneo hilo ili waweze kuchukua hatua za haraka pindi tembo wanapovamia mashamba.
Pia Mhe. Kageuka ameiomba serikali kutoa fidia kwa wakulima 23 ambao mashamba yao yameharibiwa na tembo ambapo fidia hiyo itasaidia kurudisha morali kwa wakulima na kuwapa ahueni katika kipindi hiki kigumu cha uharibifu wa mazao yao na kwamba mfumo wa fidia kwa wakulima ili kuhakikisha kuwa wanapata msaada pale wanapokumbwa na majanga ya aina hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mhe. Hassan Mkopi, amekiri kuwa tatizo la uvamizi wa tembo katika maeneo ya vijijini ni changamoto kubwa huku akisema kuwa menejimenti ya Halmashauri imepokea hoja hiyo kwa umakini na itachukua hatua stahiki.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Halmashauri Wilfred Sumari amemshukuru Rais kwa kuipatia kilosa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 150 ambapo mkataba wake umesainiwa hivi karibuni pamoja na kufufua kiwanja cha ndege chenye urefu wa kilomita 5.4 miradi hiyo itawasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa