Mkuu wa Wilaya Kilosa Adam Mgoyi Aprili 16 2018 amekemea vikali kitendo kilichofanywa na baadhi wananchi wa kijiji cha Kivungu katika kata ya Kivungu cha kuvamia shamba la mwekezaji wa Sumagro na kusababisha uvunjifu wa amani jambo ambalo si lakizalendo.
Mgoyi amesema kuwa mwekezaji huyo yupo eneo hilo kihalali, hivyo wananchi hao walipaswa kutatua kero yao ya uhitaji wa maeneo ya kulima kwa njia ya amani kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni kuliko kilichofanyika kwani wangeweza kusababisha maafa ikiwemo kupoteza uhai kwa baadhi ya watu.
‘’Uongozi wa Wilaya unasikitishwa na kulaani vikali kitendo cha uvamizi kwa mwekezaji kwani watanzania ni watu wa amani na kwamba Serikali haitalifumbia macho suala hili kwa wote waliohusika katika uvamizi huo tutahakikisha wanakamatwa na sheria kuchukua mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine’’.Mgoyi amesisitiza.
Aidha Mgoyi amewaagiza viongozi wa kata na vijiji kufanya upembuzi yakinifu wa kutambua ukubwa wa maeneo waliyonayo jambo ambalo litasaidia kujua namna ya kugawa maeneo kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo, ufugaji na uwekezaji ili kuepuka migogoro isiyo na tija.
Sambamba na hayo amewataka viongozi kuanzia ngazi ya kata, vijiji na vitongoji kutambua dhamana waliyonayo kwa wananchi kwa kuwatumikia ipasavyo ikiwemo kutatua kero ili kuachana na dhana ya kumwachia Mkuu wa Wilaya kutatua kero za wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa