Viongozi mbalimbali wa Halmashauri na Wilaya ya Kilosa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wameshiriki hatua ya awali ya ujenzi wa vituo vya afya Mikumi na Malolo kwa kushiriki kuchimba msingi wa vituo hivyo ambapo licha ya viongozi hao kushiriki Jeshi la Wananchi, wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Mikumi VETA, Wakuu wa Idara , Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi wameshiriki katika uzinduzi huo.
Akizindua ujenzi wa vituo vya afya kwa kata ya Mikumi na Malolo kwa njia shirikishi ya kuchimba msingi Mgoyi amesema kuwa viongozi hao wameshiriki katika ujenzi huo ikiwa ni njia ya kupungaza gharama za kuwalipa mafundi lakini pia kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais John Magufuli katika kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya upatikanaji wa huduma za afya kwa kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya.
Akielezea kuhusu kituo cha afya cha Mikumi Mgoyi amesema Mhe Rais wa awamu ya tano ametoa shilingi milioni 420 ili kuhakikisha kata hiyo inakuwa na kituo hicho ambacho kwa upande wa Halshauri watachangia kwa mujibu wa bajeti iliyopangwa pamoja na wananchi wakichangia nguvu kazi huku kwa upande wa kituo cha afya Malolo shirika la TAZAMA litachangia zaidi ya shilingi milioni 135 kwa ajili ya ujenzi huo .
Aidha katika uzinduzi wa ujenzi wa kituo cha afya Malolo Mkuu wa Wilaya huyo alifanya changizo ambapo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itachangia mifuko 200, Halmashauri katika bajeti yake ya 2019/20120 watatoa mifuko ya saruji 300, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ameir Mbarak ameahidi mifuko 100 ya saruji, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU wakiahidi mifuko 10 ya saruji, madiwani wa Tarafa ya Mikumi wakiahidi kuchangia mifuko 50, huku wananchi wa kata ya Malolo wakitakiwa kuhakikisha wanachangia tofari laki moja kwa vitongoji vyote vya Malolo.
Naye Mkuu wa Idara ya Afya Dkt. Halima Mangiri amesema Kituo cha Afya Mikumi wanatarajia kujenga jengo la mapokezi, maabara, wodi ya kina mama na jengo la upasuaji huku Kituo cha Afya Malolo wakijenga jengo la wodi ya wazazi, maabara na jengo la mapokezi ambapo huduma mbalimbali zitapatikana katika vituo hivyo ikiwemo upasuaji kwa kinamama walioshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida, matibabu kwa wagonjwa wa nje na vipimo mbalilmbali ikiwemo upimaji wa damu, figo na ini.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa