Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh. Majid Mwanga amewataka viongozi katika Kata na vijiji kuhakikisha michango yote inayochangishwa katika maeneo yao inakuwa na kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji kwani kumekuwa na hulka ya baadhi ya viongozi kuchangisha michango kiholela bila kufuata taratibu za upatikanaji wa kibali.
Mwanga ametoa rai hiyo wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Kitunduweta katika kata ya Mhenda ambapo amesema kuwa kumekuwa na baadhi ya viongozi wamekuwa wakikiuka taratibu za uchangishaji michango jambo ambalo si sahihi huku akitaka michango iliyokuwa inaendelea kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Mhenda kusimama mara moja kwani tayari Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa shilingi milioni 600 kwa ajili ya shule ya sekondari, hivyo hakuna haja ya mchango huo kuendelea ambapo amesisitiza kuwa hakuna michango inayozuiwa endapo itafuata taratibu za kupata kibali.
Aidha amekipongeza Kijiji cha Kitunduweta kwa namna kilivyoweza kuhifadhi vyema msitu wa kijiji uliopo katika hali ya uendelevu licha ya shughuli za uvunaji mkaa kuendelea lakini kupitia elimu na uwezeshwaji kutoka MJUMITA na TFCG msitu huo umekuwa katika hali ya uendelevu huku akitoa rai kwa TFCG kutafuta fedha kwa lengo la kufanya oparesheni maalum ya kurejesha msitu wa Ukwiva ili urejee katika hali yake ya zamani.
Akizungumzia suala la ulimaji bangi amesema wapo baadhi ya viongozi na wananchi wamekuwa wakishiriki katika kilimo cha bangi ambacho hivi karibuni Kamati ya Ulinzi na Usalama ilifanya oparesheni maalum katika misitu wa Ukwiva ambao umeharibiwa sana hususanivyamvyo vya maji ambavyo vimeharibiwa kwa kiasi kikubwa huku shughuli za kibinadamu zikiendelea ikiwemo kilimo cha bangi.
Mwanga amesema katika operesheni hiyo kamati ya ulinzi na usalama ilifanikiwa kuteketeza zaidi ya heka kumi za zao la bangi ambapo tayari wahusika wameshakamatwa na kuchukuliwa hatua huku akisema kuwa lengo la operasheni hiyo kupambana na madawa ya kulevya ya aina mbali ni sehemu ya kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais katika kupambana na madawa ya kulevya na kwamba kilimo hicho katika Wilaya ya Kilosa hakikubaliki hata kidogo kwani ulimaji bangi umekua ukichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu vijana ambao ni taifa la kesho.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa