Jumla ya vikundi 25 kutoka makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopata mkopo wa asilimia 10% toka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ikiwa ni fedha kutoka mapato ya ndani vimetakiwa kutambua thamani ya mkopo huo kwa kuhakikisha vinafanya marejesho ya fedha hizo kama inavyostahiki.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Alto Mbikiye wakati wa mafunzo kwa vikundi hivyo ambapo Halmashauri imetoa mkopo wa kiasi cha shilingi 333,192,320.00 ambapo vikundi 5 vya vijana vimepata mkopo wa shilingi 58,838,400.00, vikundi 12 vya wanawake shilingi 234,596,640.00 na vikundi 8 vya watu wenye ulemavu wakipata mkopo wa shilingi 39,757,280.00 ambazo zinapaswa kuwasaidia katika kuinua kipato chao.
Mbikiye amevitaka vikundi hivyo kufanya marejesho ya fedha hizo kwa wakati kwani mkopo huo hauna riba na kwamba kila kikundi kinapaswa kufanya marejesho kupitia namba ya malipo(control number) ambazo kila kikundi kimepewa namba ambazo ndizo zitatumika kipindi chote cha muda wa mkopo.
Pamoja na msisitizo huo vikundi hivyio vilipata mafunzo katika nyanja mbalimbali kupitia wataalam toka benki za NMB na CRDB pamoja na wataalam toka idara za biashara, kilimo na mifugo, sheria, ustawi wa jamii, TAKUKURU na Maendeleo ya Jamii, lengo ikiwa ni kuwawezesha kuendana sawasawa na maombi na makusudi ya mkopo ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Aidha wawakilishi mbalimbali toka makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu waliohudhuria mafunzo hayo ya siku moja wametoa shukrani zao kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Uongozi wa Halmashauri chini ya Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwatazama kwa jicho la tatu na kuwawezesha kwa fedha ambazo wameahidi kuzitumia kwa malengo yaliyokususdiwa na kuzirejesha kwa wakati kwani Serikali imewaamini na kwamba wanaamini zitawasaidia kuwainua katika vipato vyao na kuwaletea maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa