Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa viongozi mbalimbali wa kata kuwa watii na kuzingatia nidhamu ya utendaji kazi kwa kufuata taratibu za kazi ikiwemo kufuata taratibu zanazopangwa katika ofisi husika sambamba na kuripoti kazini kwa wakati pamoja na kusaini katika daftari la mahudhurio.
Mgoyi amesema hayo wakati alipokuwa akifanya kikao na viongozi wa kata za Msowero, Mvumi, Mbigiri, Magole, Dumila na Kitete ambapo amesema kuwa mtendaji wa kata lazima awe na taarifa za kiutendaji za watu walio chini yake, sambamba na kusimamia nidhamu na muonekano mzuri kwa wanaoongoza ikiwemo uvaaji wa staha unaozingatia nidhamu.
Sambamba na hayo Mgoyi amewataka watendaji wa kata kutambua kuwa wao ni viongozi wanaomwakilisha Mkurugenzi Mtendaji hivyo wahakikishe hawakai maofisini badala yake watoe ushirikiano mkubwa kuhakikisha changamoto, kero na ushauri unafanyiwa kazi badala ya kusubiri Mkurugenzi Mtendaji kuja kutatua kero na changamoto za wananchi.
Aidha Mgoyi amewaagiza watendaji wa vijiji kuwa na madaftari ya wakazi katika vijiji vyao ili kuwatambua wakazi waliopo na wanaongia jambo ambalo litasaidia kuepushwa kwa migogoro mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi na kwamba daftari hilo kila mtendaji wa kijiji ahakikishe liwe limekamilika pindi ifikapo Machi 30 mwaka huu, pamoja na hayo amewaagiza viongozi wote kuhakikisha chakula kinatolewa mashuleni pindi watoto wawapo mashuleni kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa