Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale ametoa wito kwa viongozi wa ngazi mbalimbali wa kiserikali na kidini walioko wilayani Kilosa kuungana kwa pamoja kuendelea kujenga msingi imara juu ya uelewa wa udhibiti wa maambukizi ya virusi vya covid 19 lengo ikiwa ni kuhakikisha wilaya inakuwa salama kwani mpaka sasa baadhi ya wananchi wameendelea kuchukua hatua za awali wa kuweka ndoo na sabuni katika maeneo yao licha ya kwamba kuna baadhi ya wananchi hawako tayari kunawa mikono ikiwa ni sehemu mojawapo ya kujikinga na virusi vya corona.
Mwambambale amesema kuwa yapo baadhi ya maeneo watu wameweka ndoo za maji lakini zikiwa hazina maji na maeneo mengine ndoo zina maji lakini watu wamekuwa hawataki kunawa na kwamba kunawa kwa kipindi hiki cha maambukizi ya corona ni suala la lazima hivyo amewataka viongozi hao kuendelea kusimamia maagizo yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu na kwamba hadi sasa ugonjwa wa corona upo katika maambukizi ya ngazi ya kijamii hivyo ni vema watu wakaendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo ya viongozi na wataalam wa afya wanavyoelekeza.
Aidha amesisitiza viongozi hao kuhakikisha michezo mbalimbali inayokusanya watu wengi kwa wakati ambayo ni vigumu kuzingatia taratibu za udhibiti wa kusambaa kwa virusi vya covid 19 kama vile uchezaji wa mpira wa miguu unaondelea katika maeneo mbalimbali ameelekeza kusitishwa kwa mechi hizo sambamba na mazoezi mbalimbali yanayohusisha mkusanyiko, huku akisisitiza kusimamishwa kwa vibanda mbalimbali vinavyoonyesha picha mbalimbali za video almaarufu kama vibanda umiza ambavyo kwa asilimia kubwa vinahusisha mikusanyiko ya watoto na watu wazima pamoja na kutohusishwa kwa watoto katika kutembeza biashara mbalimbali mitaani.
Akibainisha maagizo muhimu ya kutekeleza katika tarafa, kata, vijiji na nyumba za ibada ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona Mkuu wa Idara ya Afya Kilosa Dkt. George Kasibante amesema maafisa tarafa, watendaji wa kata na vijiji wanao wajibu wa kuhuisha na kusimamia Kamati za Afya za kata na vijiji, Kusimamia maeneo yao kwa kuhahakisha kanuni zote za kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) zinafuatwa, Kuzuia mikusanyiko kwenye pull table, mashine za bahati nasibu(slots machines), mabanda ya video, vilabu vya pombe, baa, minada, harusi, misiba na maeneo ya kutolea huduma mbalimbali, Kuhakikisha baa na vilabu vya pombe wanafungua baada ya muda wa kazi, kuhakikisha kunakuwepo na ndoo za maji tiririka na sabuni za kunawia mikono kwenye maeneo ya biashara na nyumba za kuishi.
Pia kuhakikisha wananchi wa maeneo yao wanapunguza safari zisizo za lazima, Kuwafatilia na Kuwatambua wageni wanaoingia na kuwaripoti kwenye mamlaka husika wanapokua na wasiwasi na afya zao, Kutoa ripoti kila siku ya elimu ya afya kwenye maeneo yao, Kufanya ukaguzi na utekelezaji wa hatua za kujikinga na maambukizi ya Corona hasa maeneo ya mikusanyiko, Kuwachukulia hatua wale wote ambao hawataki kufuata taratibu zilizotolewa, Kutoa elimu kwa viongozi na wananchi kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19). – WDC, Halmashauri, Kuzuia michezo inayokusanya watu wengi kwa wakati mmoja na ambayo ni vigumu kuzingatia taratibu za kudhibiti na kuingiza ajenda ya COVID-19 katika vikao vyao kwenye ngazi mbalimbali.
Kwa upande wa viongozi wa dini Dkt. Kasibante amesema wanao wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na ndoo za maji tiririka na sabuni kwenye nyumba za ibada wanazoziongoza, Kuweka mtu maalumu atakayesimamia uwepo wa maji na sabuni na kuhakikisha watu wote wanaongia na kutoka kwenye nyumba za ibada wana nawa mikono yao, Kuhakikisha watu wanakuwa mbalimbali (mita 1) wakati wa maandalizi ya ibada na wakati wa kufanya ibada, Kufupisha muda wa kufanya ibada kwa baadhi ya madhehebu, Kuingia kwa awamu ya watu wachache kufanya ibada kwa baadhi ya madhehebu ili kupunguza mkusanyiko au msongamano, Kupulizia dawa kwenye nyumba za ibada baada ya ibada kuisha na kupokea mapendekezo ya viongozi wa dini juu kujikinga na ugonjwa wa COVID.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa