Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga ametoa rai kwa viongozi wa dini kuendlea kuhubiri amani katika nyumba za ibada huku wakiendelea kuvumiliana wakati uongozi ukiendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizopo ndani ya wilaya.
Mwanga ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini zote Kilosa ambapo amesema ili kukabiliana na changamoto ni wajibu wa kila kiongozi kutafuta majawabu ya changamoto hizo kwa kuwa na uongozi wa pamoja huku akisema endapo zitapatiwa majawabu hakutakuwa na mabango, huku akisisitiza viongozi hao kuzungumzia mazuri na vivutio vilivyopo ndani ya wilaya ili kuvutia wawekezaji jambo litakalosaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana waliopo Kilosa.
Akizungumzia suala la ulinzi amesema ulinzi uko katika maeneo mbalimbali ambapo kwa upande wake amesema kila mmoja analo jukumu la kumlinda mtoto wa kike ambaye kwa asilimia kubwa anakumbana na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kupelekea kutofikia ndoto zake, hivyo anapaswa kuwezeshwa kujitambua, kujiamini na kujithamini, huku upande wa vijana akisisitiza walindwe dhidi ya madawa ya kulevya pamoja na kukemea utoro mashuleni.
Kwa upande wa mashamba yaliyofutwa amesema upo utaratibu unaoendelea kufanyika hivyo wasiwe na wasiwasi kwani baada ya taratibu stahiki kukamilika mchakato wa ugawaji utakuwa wa wazi bila kificho huku akiahidi kufanya ziara za kutembelea vijiji vyote na kukutana na viongoz ili kuweka mkakati na kujenga uelewa wa pamoja lengo ikiwa ni kufanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu huku wakimtanguliza Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa na viongozi hao wa dini ni migogoro ya wakulima na wafugaji jambo linalopelekea hali ya uzalishaji na kipato kushuka, kukosa uendelevu wa maeneo muhimu, kutokarabatiwa tuta la mto Mkondoa, uhaba wa mashamba, kutopatikana kwa zaka ya kutosha katika nyumba za ibada kutokana na waumini kushinda mashambani kwa kuhofia kulishiwa mashamba yao na wafugaji wakiwa nyumba za ibada, wakulima kupigwa na wafugaji pamoja na migogoro ya ardhi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa