Waheshimiwa madiwani na Watendaji wa kata wametakiwa kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vilivyopo katika maeneo yao vinakusanywa kwa kadri inavyostahiki ili kuiwezesha Wilaya ya Kilosa kuwa na mapato ya kutosha ili kujiletea maendeleo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kilosa Mh. Wilfred Sumari ambapo ametaka kila kiongozi katika eneo lake kusimamia vema vyanzo hivyo ili Wilaya iweze kuendesha shughuli zake pamoja na kujiletea maendeleo.
Akizungumzia zoezi tarajiwa la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 amesema kupitia sensa ndipo takwimu sahihi za kiwilaya hupatikana ambapo ametaka wananchi kuhamasishwa kushiriki zoezi hilo ili kupata takwimu sahihi kwaajili ya kupanga mipango ya maendeleo na upatikanaji wa huduma hizo hupangwa kulingana na idadi ya watu hivyo ni vema ikafanyika hamasa ya kutosha.
Aidha amesisitiza wananchi kuendelea kupata chanjo ya uviko-19 ili kujikinga huku akiwataka viongozi mbalimbali kuendelea kuwahamasisha wananchi ili kufanikisha zoezi la chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka mitano.
Sumari amewaomba viongozi wote kuendelea kushirikiana katika kuijenga Kilosa kwa kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika kata mbalimbali huku wakizingatia ushauri wa kisheria na kitaalam pamoja na kusimamia sheria ndogo zilizopitishwa ili zitumike katika vijiji kwa mustakabali wa maendeleo ya wananchi wa Kilosa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba amesisitiza vikao na mikutano itakayofanyika katika kata na vijiji ajenda ya zoezi la sensa ipewe kipaumbele ili kuwajengea wananchi uelewa na hamasa ya kushiriki zoezi hilo huku akibainisha faida za sensa ikiwemo wilaya kupata fedha za maendeleo kwa mujibu wa idadi ya watu, kuinua shughuli za kiuchumi ambapo ametoa rai kwa vijana kuomba nafasi za kazi kwa ajili ya zoezi hilo ambalo mchakato wa maombi mwisho ni Mei 19, 2022.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa