Viongozi wa tarafa, kata na vijiji wametakiwa kutimiza majukumu yao kwa kufanya kazi zao ikiwemo kusimamia maeneo yao na kuhakikisha amani inakuwepo hususani katika kukabiliana na migogoro katika kipindi cha kiangazi na msimu wa maandalizi ya mashamba.
Rai hiyo imetolewa Septemba 11 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati wa kikao chake na viongozi wa tarafa za Masanze, Ulaya, Kilosa mjini na Kimamba ambapo amewataka viongozi hao kutokuwa chanzo cha migogoro katika maeneo yao kwa kuhakikisha vikao vya amani na vya kisheria vinafanyika sambamba na kutopokea mifugo kiholela jambo linalosababisha mifugo kuongezeka kwa wingi.
Mgoyi amesema viongozi hao wanao wajibu wa kusimamia na kuhakikisha migogoro inaisha na kwamba suala hilo linahitaji uwajibikaji na yeyote ambaye ataonesha kutowajika ipasavyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake huku akiwataka kuhakikisha wanahakiki idadi ya mifugo jambo litakalosaidia kutambua mifugo vamizi katika maeneo yao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale ametoa onyo kwa viongozi hao kuacha mara moja hulka ya kukaribisha wageni kwa makubaliano yasiyo rasmi jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro huku akiwataka kufanya kazi kama timu na kuendesha shughuli zao kwa kufuata taratibu kanuni na sheria jambo litakalowasaidia kufanya kazi katika njia sahihi kwani serikali za vijiji ni mamlaka ambazo zinaweza kupokea changamoto na kuzimaliza kwa mujibu wa taratibu ikiwemo umalizaji kwa njia ya vikao.
Aidha Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila amewataka viongozi hao kusimamia na kutekeleza maazimio yote yaliyotokana na kikao hicho ikiwemo utekelezaji wa agizo lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ndani ya siku saba takwimu za idadi ya mifugo ziwe zimepatikana kwa kila eneo lakini pia kufanyika kwa tathmini za ukweli, sambamba na wenyeviti wa vijiji kutimiza wajibu wao, kukaa vikao vya kisheria, kutatua migogoro kwa kutafuta chanzo cha tatizo pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa