Viongozi mbalimbali wilayani Kilosa wametakiwa kuzingatia zaidi maadili katika utendaji wa kazi za kila siku kwa kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za majukumu yao ya kila siku katika kuwatumikia wananchi.
Rai hiyo imetolewa Juni 5, 2023 na Afisa Maadili Kanda ya Mashariki Bw. Selemani S. Selemani wakati akizungumza na baadhi ya waheshimiwa madiwani pamoja na wakuu wa idara na vitengo ikiwa ni sehemu ya kukumbushana suala zima la maadili na uwajibikaji katika sekta ya Umma ambapo amesema viongozi wanapozingatia maadili inapelekea kuwepo kwa amani na uadilifu.
Selemani amesema kuwa katika kuhakikisha uwajibikaji unachukua nafasi yake ipo misingi ya uwajibikaji ambayo inapaswa kusimamiwa na kila mmoja ikiwemo kufanya maamuzi kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu, kupokea maoni na ushauri kama fursa ya kuboresha utendaji kazi, kufanya tathmini na kuendelea kujifunza kutokana na uzoefu, kupitia upya mifumo ya taasisi na kufanya maboresho ili kuendana na mabadiliko ya mazingira na kuongeza ufanisi na ubora, kuwa na kiu ya kufanya mambo katika ubora na endelevu pamoja na kujenga tabia ya ushirikiano.
Akibainisha aina za uwajibikaji amesema zipo aina kadhaa za uwajibikaji ikiwemo uwajibikaji binafsi, uwajibikaji wa kitaaluma, uwajibikaji wa kifedha, uwajibikaji wa kimaadili, uwajibikaji wa kiutawala na wa kampuni, huku akisema upo umuhimu wa wa uwajibikaji ikiwemo uwepo wa matumizi bora ya rasilimali za umma ili kufikia malengo ya Taifa, kudumisha uwazi katika utekelezaji na taratibu za kutoa maamuzi, kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa, kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka, kutenda haki pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi na Serikali yao.
Sambamba na hayo amesema katika kusimamia uwajibikaji zipo changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na imani na watumishi, kufanya kazi kwa mazoea, hofu ya kushindwa, ukosefu wa mawasiliano na ushirikiano kati ya kiongozi na watumishi pamoja na kutopenda ama kukosa muda wa kuendeleza watumishi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa