Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred .L. Sumari amewataka Viongozi kuanzia ngazi ya kijiji na kata kubeba jukumu la kuwatangazia wananchi mapato na matumizi ili waweze kutambua kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita.
Hayo yamesemwa Novemba 15,2023 katika ukumbi wa Chuo Cha Maendeleo (FDC) Ilonga kwenye Mkutano wa kawaida wa baraza la Madiwani wa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mhe. Sumari amesema kuwa fedha nyingi zinazokuja katika Halmashauri zinaenda katika ngazi ya kijiji na kata hivyo ni wajibu wa kila Mwananchi kufahamu mapato na matumizi katika kijiji husika ambapo hali hii itapelekea ufahamu wa kujua shughuli mbalimbali za maendeleo yanayotekelezwa katika serikali ya awamu ya sita.
Sambamba na hayo pia Mhe. sumari amewataka wahe. Madiwani, watendaji wa kata na vijiji kuendelea kutoa ushirikiano kwa kusimamia vema hali ya uhifadhi wa Mazingira na vyanzo vya maji ambapo wakulima wamekuwa wakilima mazao yao kando kando ya vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka Wahe. Madiwani kusimamia vema miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita katika kata zao.
Mhe. Shaka ameeleza kuwa ni vema wahe. Madiwani wajenge utamaduni wa kuzungukia Miradi ya maendeleo katika kata zao pia kuwasomea wananchi taarifa ya miradi inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
Pia Mhe. Shaka ameongeza kuwa wahe. Madiwani wahakikishe Halmashauri kupitia jitihada za wataalamu miradi inakamilika kwa wakati na ajira zilizozalishwa katika miradi hiyo wanufaika ni wananchi wa kata husika.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa