Waajiriwa wapya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wamepatiwa mafunzo elekezi yaliyolenga kuwaandaa katika majukumu yao mapya.
Mafunzo hayo yametolewa 06 Januari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ambapo mafunzo hayo yamehusisha mada muhimu zinazohusu maadili ya kazi, uwajibikaji, kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Akizungumza katika kikao hicho Afisa Utumishi Ndg George Lazaro aliwataka waajiriwa wapya kutumia mafunzo hayo kama msingi wa utendaji bora na nidhamu kazini. Aliwasisitiza kuwa wanapaswa kujitahidi kuwa waadilifu, wabunifu, na kushirikiana na wenzao kazini ili kuimarisha huduma bora kwa wananchi.
"Ninyi ni kundi jipya la watumishi mnaoingia kwenye mfumo wa halmashauri tunategemea mchango wenu mkubwa katika kuboresha huduma na maendeleo ya jamii yetu. Tunataka kuona nidhamu, uwajibikaji, na juhudi za dhati katika kila mnachofanya," alisema Lazaro.
Kwa upande wake Afisa Utumishi Ndg.Hussein Ayoub, aliwaeleza waajiriwa kuhusu haki na wajibu wao kama watumishi wa umma, akiwakumbusha kuwa utumishi wa umma ni dhamana kubwa inayohitaji uadilifu na weledi. Alieleza kuwa kwa kufuata maadili ya kazi na taratibu zilizowekwa wataweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kusaidia kufanikisha malengo ya halmashauri. "Tunawapa nyenzo za msingi za utumishi mnapaswa kuzingatia miongozo hii ili kufanikisha kazi zenu kwa weledi," alisema Ayoub.
Katika mafunzo hayo waajiriwa wapya walipata nafasi ya kuuliza maswali na kushiriki mijadala kuhusu changamoto mbalimbali wanazotarajia kukutana nazo. Mafunzo hayo yaliibua mijadala yenye tija kuhusu namna bora ya kushirikiana kazini na kutoa huduma bora kwa wananchi. Mafunzo hayo pia yalilenga kuwaelekeza waajiriwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za utumishi wa umma na taratibu za kiutawala.
Naye Yamola Elias Daga mmoja wa waajiriwa wapya, alitoa shukrani kwa uongozi wa halmashauri kwa kuwaandalia mafunzo hayo muhimu. Alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuelewa vyema majukumu yao mapya na yatawajengea uwezo katika majuku yao ya kila siku. "Tunaishukuru sana halmashauri kwa mafunzo haya tumepata maarifa mengi ambayo yatatusaidia kufanya kazi kwa weledi na ufanisi," alisema Yamola.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa