Ili wananchi walime kwa tija tunahitaji kufanya mabadiliko ya kifikira , namna ya utendaji na mfumo kwani mkoa wa Morogoro ni mkoa wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania ukiwa na ongezeko kubwa la watu na eneo kubwa, lakini pia ni mkoa wenye migogoro mingi ya ardhi kutokana na watendaji kushindwa kusimamia wananchi vizuri katika matumizi ya ardhi ipasavyo.
Hayo yamebainishwa Septemba 28 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Fatma Mwassa wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa Kilimo likiwa na lengo la kuongeza hamasa kwa vijana kutambua kuwa Kilimo ni fursa katika kujipatia kipato na kujiajiri kwa kauli mbiu inayosema “TUNAANZIA SHAMBANI”.
‘‘Licha ya ukubwa mkoa wa Morogoro wenye ardhi yenye rutuba mkoa umekuwa haufanyi vizuri katika uzalishaji mfano zao la mpunga unazalishwa kwa wastani wa tani 2.3 kwa ekari badala tani 6, mahindi tani 1.5 kwa ekari badala ya 6, viazi ni tani 2.6 badala ya tani 20 na ndizi tani 4.4 badala ya tani 35 na miongoni mwa sababu za uzalishaji usio na tija ni kilimo cha kutegemea mvua, matumizi ya mbegu za kienyeji, kutotumia mbolea au mbolea isiyo sahihi, kutokujua hali ya udongo na mazao inayostawisha pamoja na tabia ya watu kutenga eneo kubwa bila kujali uwezo wa kulihudumia ambapo kutokana na changamoto ya mvua na uzalishaji usio na tija mkoa umeamua kuchukua hatua za makusudi kuwa na kongamano ambalo litatupa fursa ya kujifunza, kutathmini na kuamua kwa pamoja nini kifanyike’’. Amesema Fatma Mwassa.
Wadau walioshiriki katika kongamano ni wabunge, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, wakulima, wauza zana za Kilimo na pembejeo na taasisi za Serikali kama TFS, NEMC, TAWA, TANAPA, na nyingine lengo ikiwa kujadili kwa pamoja namna ya kuondoa changamoto za kilimo zinazotokana na mwingiliano wa shughuli zinazofanyika na wadau husika.
Aidha uwepo wa kongamano hilo utaambatana na tukio la uzinduzi wa msimu wa Kilimo 2022/2023 kimkoa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 3 mwaka huu katika Wilaya ya Kilosa ambapo jumla ya Ekari 5496 zitagawiwa kwa wakulima ikiwa ni sehemu ya ardhi inayotokana na mashamba tisa (9) ambayo umiliki wake ulibatilishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuona mashamba hayo hayaendelezwi ambapo mashamba yanategemewa kupunguza uwepo wa migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kongamano hilo Mh. Prof. Palamagamba Kabudi amesema uwepo wa kongamano hilo ni fursa nzuri ya utekelezaji wa shughuli za kilimo kwani mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kipekee kwa shughuli za kilimo kutokana na ardhi iliyopo huku akimshukuru Mheshimiwa Rais kwa msukumo mkubwa aliouweka katika kilimo ikiwemo kuwezesha ujenzi tarajiwa wa skimu mbili kubwa katika mkoa wa Morogoro ambapo moja inatarajiwa kuwepo katika wilaya ya Kilosa katika kata ya Rudewa.
Pro. Kabudi amesema uwepo wa kongamano hilo litatoa mwelekeo wa namna ya kuendesha sekta ya kilimo ili kusukuma mbele maendeleo ya taifa kwani mkoa wa Morogoro una neema ya kuwa na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo na kwamba anaamini kupitia dhana ya siasa ni kilimo, kilimo kinapaswa kuwezesha upatikanaji wa mahitaji ya chakula kwa ajili ya wakulima na wasiolima, upatikanaji wa mazao ya kuuza nje na kuzalisha kwa ajili viwanda na kwamba kupitia kongamano hilo yatapatikana maazimio ambayo yanapaswa kutekelezwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa