Juni 3 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa wafanyabiashara kuwa wabunifu kwa kutengeneza mifuko mbadala ili kuepuka kupoteza wateja kutokana na uhaba wa mifuko uliopo sasa baada ya kuwepo katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imebainika kuwa na athari kimazingira na kwa mifugo.
Mgoyi ametoa wito huo wakati wa zoezi la ukaguzi wa utekelezaji wa kuondoa mifuko ya plastiki madukani ambapo amewataka wafanyabiashara kuwa wabunifu ikiwemo kutengeneza mifuko kwa kutumia magazeti ili kutopoteza wateja kutokana na kukosa mifuko ya kuhifadhia bidhaa pia amewashukuru wafanyabishara kuitika zoezi hilo huku akitoa mwaliko kwa wafanyabiashara wakubwa kutengeneza mifuko na kuisambaza kwani ipo changamoto kubwa ya upatikanaji wa mifuko mbadala.
Kwa upande wa wafanyabiashara Mary Lyanzile na Hassan Kombo almaarufu mpemba wamesema pamoja na kuitika zoezi hilo wanakumbana na changamoto kubwa ya uhaba wa mifuko ambayo hupelekea kukosa wateja na kusababisha mapato yao kushuka lakini pia wamesisitiza kuongezwa kwa kiwango cha ubora wa mifuko kwani iliyopo kwa sasa inaonekana kukosa ubora, sambamba na hayo wametoa wito kwa wateja wao kutumia mifuko ya visalfeti inayoonekana kuwa imara pia wamepongeza usafi wa mazingira ambao umeanza kuonekana kwa baadhi ya maeneo ambapo mifuko ilikuwa ikizagaa.
Naye Janelove Thobias mfanyabiashara wa soko la Sabasaba amesema ni vema kwa mazingira yaliyopo sasa wafanyabiashara hasa wa sokoni wakajiongeza na kutengeneza mifuko nafuu ambayo ni gharama rahisi ili kutopeteza wateja kwani mifuko hiyo ni rahisi kutengeneza na haichukui muda mrefu kuitengeneza kwakuwa unatengeneza kwa kutumia gundi na magazeti ama makaratasi yaliyotumika.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa Nathan Kaunda amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu kwani kila siku takwimu za uwasilishaji mifuko zimekuwa zikiendelea kukusanywa kutoka katika kata zote na kwamba mifuko yote inayowasilishwa inakusanywa kwa ajili ya hatua nyingine zaidi ambapo Afisa Mazingira na Udhibiti takangumu Aloyce Simeono amesema hadi sasa mifuko 11,000/ imekwisha kukusanywa kutoka katika maeneo mbalimbali ambayo imesalimishwa katika kata mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa