Rai imetolewa kwa wafanyabiashara wilayani Kilosa kuwekeza zaidi katika Wilaya ya Kilosa kwa kuongeza nguvu ya kuziona fursa za utalii na uwekezaji zaidi ili wilaya iweze kupata maendeleo na kunyanyua mji wa Kilosa.
Rai hiyo ameitoa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara waliopo Kilosa ambapo amesema ipo haja ya kutumia fursa zilizopo kwa kuwekeza zaidi jambo litakalosaidia kupunguza kasi ya ukosefu wa ajira huku akiwataka wafanyabiashara hao badala ya kutangaza migogoro watangaze fursa zilizopo.
Mwanga amesema Serikali ya Wilaya ya Kilosa ipo tayari kushirikiana na wanyabiashara watakaotaka kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo kwani wilaya inazo fursa nyingi na hali ya kijiografia iliyopo ni nzuri hivyo hata migogoro iliyopo inaweza kugeuzwa kuwa fursa.
Akiongeza fursa nyingine zilizopo ni uwepo wa mifugo mingi ambayo inaweza kuvunwa na kuhifadhiwa vizuri na kuiuza maeneo mengine, huku akisema kuwa ipo fursa ya kuwa mfano wa kuigwa ambapo vijana wanaweza wakaiga kutoka kwa wafanyabiashara hao waliofanikiwa jambo litakalowasaidia kujiongeza na kufanya biashara.
Pamoja na hayo amesisitiza suala la ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati jambo litakalosaidia mapato yatokanayo na kodi kuleta maendeleo kwa kufanya miradi mbalimbali huku akisisitiza suala la usafi kwa kila mfanyabiashara katika eneo lake ahahakishe anaweka chombo cha kuhifadhia taka sambamba na kuwakumbusha suala la usafi kwa kuweka maeneo yao ya biashara katika hali ya usafi.
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili na kukwamisha ukuaji wa biashara wafanyabiashara hao wamesema ni wingi wa tozo na kodi, kutopata msaada wa karibu toka jeshi la zimamoto, baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi kwa kutumia vitambulisho vya wajasiriamali huku wakiwa hawastahili, miundombinu mibovu ya barabara, kufungiwa biashara, kutokuwepo maelewano mazuri baina ya wafanyabiashara na Halmashauri, kutosomwa kwa mapato na matumizi, uchimbaji wa madini kiholela unaopelekea uchafuzi wa mazingira, kuhatarishwa kwa maisha ya watu kutokana na taka zinazotupwa eneo Magomeni na kutoboreshwa masoko.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa