Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mwambambale ametoa rai kwa wafanyabiashara waliopanga katika vibanda vya biashara vinavyomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa vilivyopo katika kata ya Kasiki waliofunga maduka kufungua maduka hayo ili wananchi waendelee kupata huduma.
Rai hiyo imetolewa Februari 9 mwaka huu baada ya wafanyabiashara katika eneo la soko Uhindini kuamua kufunga maduka kwa lengo la kuitaka Halmashauri iwapunguzie tozo la kodi ya kibanda kutoka shilingi 50,000 hadi 30,000 kwa mwezi kwa kibanda.
Mwambambale amesema kuwa wafanyabiashara ikiwa wana hoja za kutaka mabadiliko ya tozo hiyo njia sahihi ya kufikisha ujumbe kwa mamlaka husika ni kuifikisha hoja eneo husika ili ijadiliwe na kufanyiwa maamuzi badala ya kusitisha huduma kwa wananchi.
Amesema kuwa tozo ya shilingi 50,000 kwa kila kibanda ni tozo halali ambayo ilijadiliwa katika vikao vya kisheria hivyo ili mabadiliko yaweze kufanyika ni lazima vikao vya kisheria vifanyike na kuridhia mabadiliko hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kilosa Edward Maminya amesema kuwa zaidi ya vibanda 200 vimefungwa ili kusubiri uongozi wa juu hasa wa mkoa kuja kuwasikiliza na kutatua mgogoro huo ambapo amesema wafanyabiashara wanahitaji kulipa tozo la shilingi 30,000 kwa mwezi kulingana na gharama ya uendeshaji kuwa kubwa kuliko mzunguuko wa fedha inayopatikana katika biashara.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa