Jamii ya wafugaji wilayani Kilosa imetakiwa kuachana na dhana ya utoaji rushwa pindi mifugo yao inaposababisha athari kwenye mashamba na badala yake watumie fedha hizo kujenga shule na zahanati ili kusogeza karibu huduma za elimu na afya katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa Machi 13, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaj Majid Mwanga wakati wa kikao cha viongozi wa wafugaji ambapo ametaka jamii hiyo kujikita zaidi katika kudumisha amani kwa kuhakikisha mifugo yao inakuwa katika uangalizi mzuri ili kuepuka migogoro ambayo husababisha kutokuwepo kwa maelewano baina ya wakulima na wafugaji.
Mwanga amesema suala la kudumisha amani ni la kila mmoja hivyo kila mmoja anao wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama vinatawala ili kuifanya Kilosa kuwa ya burudani kwa mkulima na mfugaji kwa kufanya shughuli zake kwa amani na usalama.
Aidha amekemea vikali tabia ya baadhi ya wazazi kuwakatisha masomo wanafunzi kwa sababu mbalimbali na kwamba hatamfumbia macho mzazi na yoyote atakayehusika katika kumkatisha mwanafunzi masomo kwani watoto wote wana haki ya kupata elimu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Zakhia Fandey amesisitiza jamii hiyo kushiriki kikamilifu katika zoezi la Anwani za Makazi linaloendelea sambamba na kushiriki sensa ya watu na makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Morogoro Shambakubwa Longido ameuomba uongozi wa Wilaya kuikumbuka jamii ya wafugaji hususani katika mashamba yaliyofutwa huku akiomba wafugaji wote watakaobainika kulishia mifugo kwenye mashamba ya watu pamoja na watakaobainika kutopeleka watoto shule wachukuliwe hatua ili kutoipaka matope jamii hiyo na kuwa funzo kwa wengine.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa