Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka Wafugaji nchini kuingia kwenye mfumo wa ufugaji wa kisasa na wa kibiashara ili kuleta tija na kuondoa adha ya migogoro kati ya wafugaji na wakulima ambayo inaonekana kuwa ni tatizo la kudumu wilayani kilosa na sehemu nyingine zenye idadi kubwa ya wafugaji.
Mhe. Ulega ametoa agizo hilo Julai 4, 2023 katika ziara yake ya kutembelea shughuli za kimaendeleo katika ranchi ya Mkata ambapo amesema kuwa Serikali imekuja na mpango wa kuandaa program maalum ya kutoa vitalu kwa wafugaji ambapo mfugaji atakodishwa eneo maalum lenye miundombinu kwa ajili ya malisho ya mifugo kwa muda maalum kisha mifugo iyo itaingia sokoni kwa ajili ya biashara kwa kufanya hivyo kutasaidia kutanua soko la mazao ya mifugo nje ya nchi, kupata mitaji kwa maana ya kukopesheka na taasisi za fedha na kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima.
Sambamba na hayo Mhe. Ulega amesema kuwa serikali imelenga kutoa elimu ya shughuli za kimaendeleo katika sekta ya ufugaji kwa vijana hususan wazawa ambao baada ya mafunzo hayo watakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza elimu hiyo katika ngazi ya familia na jamii nzima kwa ujumla na kuleta mabadiliko chanya.
Pia Mhe. Ulega amesema kuwa mara baada ya vitalu hivyo kukamilika ni marufuku wafugaji kuvamia maeneo ya vitalu vitakavyotolewa na serikali na kusisitiza kuwa sheria kali zitachukuliwa kwa yeyote atakaye kiuka agizo hilo .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema lengo lao ni kuwafanya wafugaji wa Mkoa wa Morogoro wafanye ufugaji wa kisasa na wa kibiashara na kwamba ana amini kuwa kwa kufanya hivyo migogoro ya wakulima na wafugaji itakuwa historia Mkoani hapa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa