Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Mashimba Ndakiamewataka wafugaji kubadilika kwa kuacha ufugaji wa mazoea kwa kutegemea ardhi ya kuhama hama na badala yake wawe na eneo la kufugia mifugo yao ambalo litakuwa linatambulika kisheria.
Mh. Ndaki amesema hayo Januari 26, 2023 katika kata Madoto na Ulaya katika ziara ya kikazi ambapo amewataka wafugaji kuacha tabia ya kulishia mifugo katika mashamba ya wakulima jambo linalopelekea migogoro isiyoisha baina ya wakulima na wafugaji.
Sambamba na hayo amewataka wafugaji na wakulima kushirikiana katika shughuli zao na kuacha kuvutana kwani kufanya hivyo itapelekea kurudisha maendeleo nyuma.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mh. Palamagamba Kabudi amesema Wilaya ya Kilosa ni kubwa ikiwa na shughuli nyingi za kiuchumi, hivyo ni vema yakatengenezwa mazingira ya kuwasaidia wafugaji kupata mafunzo kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo ili ziweze kutoa mafunzo kwa wafugaji na kuwahamasisha kufuga kisasa kwa kunenepesha mifugo ili iweze kuleta tija,lakini pia upo uhitaji mkubwa wa malambo na majosho ya mifugo ili waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo sambamba na mafunzo ya ufugaji wa kibiashara.
Aidha ameiomba Wizara ya Mifugo kuwahamasisha wafugaji kulima pamoja na kufuga kisasa ili mifugo iweze kuwa na kiwango kizuri cha ushindani wa soko lakini pia kuwahamasisha wananchi juu ya ufugaji wa samaki jambo litakalosaidia wananchi kujiongezea kipato huku Mwenyekiti wa Hamashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh. Wilfred Sumari akiuomba vitalu vya lanchi ya Narco vilivyogawiwa kwa wawekezaji lakini haviendelezwi kurudishwa kwa wananchi ili wapatiwe kwa ajili ya shughuli za ufugaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo amemshkuru Mh. Waziri kwa kufika Kilosa ambapo amesema wafugaji na wakulima wanatakiwa kufuga kibiashara kwa kufuga mifugo yenye tija kwenye soko kila ndani na nje ambalo litaendana na mabadiliko ya tabia nchi.
Dkt. Yuda amesema kwa sasa maeneo ya malisho yamezidi kupungua hivyo wajitahidi kuwa na maeneo ambayo yatasaidia kwa ajili ya malisho ili kuondoa ama kupunguza migogoro isiyo ya lazima ili kufanya maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa