Waganga Wafawidhi Wilayani Kilosa wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili waweze kuboresha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari wakati akizungumza na Waganga Wafawidhi katika kikao cha kuwajengea uwezo waganga hao kilichofanyika Septemba 13, 2024 katika ukumbi wa Maktaba yaHospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Mhe. Sumari amewataka Waganga hao kufanya kazi kwa ushirikiano na kusaidiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeleta fedha nyingi katika Halmashauri ya wilaya ya Kilosa kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa kuna haja ya kushirikisha ngazi zote za uongozi kuanzia uongozi wa kijiji na wataalamu wote katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan miradi ya afya ili iweze kukamilika kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Pia Mhe.Sumari amebainisha kuwa ukusanyi wa fedha bila kuingiza kwenye mfumo husika ni kosa la jinai hivyo, amewasihi watumishi hao kufuata sheria, kanuni na taratibu za serikali katika kusimamia ukusanyaji wa mapato.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael J Gwimile amewataka Waganga hao wa vituo kusimamia suala zima la ukusanyi wa mapato na kuwakumbusha kuwa ni wajibu wa kila mtumishi kushiriki katika kukusanya mapato.
Sambamba na hayo, Ndg. Gwimile ameeleza kuwa ni vyema kushirikishana katika changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili ziweze kutatuliwa kwa wakati ili kuboresha na kutoa huduma bora kwa wananchi katika sekta ya hiyo ya afya.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa