Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mussa Ali Musa amewataka Wahandisi wa majengo kufanya kazi Kwa weredi ili kuikamilisha miradi Kwa wakati uliopangwa huku akiwataka kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Ameyasema hayo katika kikao cha pamoja cha majumuisho ya miradi ya ujenzi kilichofanyika katika Halmashauri ya Kilosa Disemba 7, 2023 na kujumuisha Halmashauri zote za mkoa wa Morogoro lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja na pia kujifunza teknolojia mpya zinazojitokeza kwenye sekta ya ujenzi.
Ameongeza kuwa baadhi ya Wahandisi hawafiki kuikagua miradi mara kwa mara huku wengine hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa wale wanaosimamia na wanaotekeleza miradi hiyo wakiwemo mafundi na kuwataka waandae mipango kazi Ili kurahisisha kazi zao.
Aidha amewashauri Wahandisi kuhakikisha wanajenga hifadhi za maji katika miradi mipya husasani kwenye shule hasa za bweni Ili zirahisishe uzimaji wa moto endapo likitokea Janga la moto kwenye majengo hayo.
Katika kuzijibu changamoto wanazokumbana nazo Wahandisi hao katika kutekeleza majukumu yao, amezitaka mamlaka za kiutawala kuwapa ushirikiano Wahandisi hao huku akiwataka Wahandisi kuwa wabunifu katika kazi zao.
Kwa upande wake Mhandisi Mkuu wa Mkoa Mhandisi Ezron Kilamhama ambaye ndiye muandaaji wa kikao hicho, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kutambua hatua zilizofikiwa katika miradi mbalimbali kwa Halmashauri zote za mkoa lakini pia kubadilishana uzoefu baina ya Wahandisi wote na kuongeza kuwa utaratibu huu hufanyika Kila mwaka ambapo huchaguliwa Halmashauri mojawapo ya kufanyai kikao h icho.
Wakiwasilisha taarifa zao za miradi ya ujenzi, Wahandisi wa Halmashauri zote wamebaisha kuwa ipo miradi iliyokamilika, ambayo haijakamilika na Ile iliyoko katika hatua za mwisho huku wakibainisha changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro Juma M. Gwiso amesema kuwa miradi mbalimbali imetekelezwa katika Manispaa hiyo ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari kata ya Boma, ujenzi wa soko la wamachinga fire, ujenzi wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari Kilakala, ujenzi wa bwalo la chakula Fungafunga, ujenzi wa kituo cha afya kata ya Tungi, ujenzi wa madaraka manner shule ya sekondari Morogoro na ujenzi wa Barabara zenye urefu wa kilometa 12.85
Naye muwasilishaji kutoka katika Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Miundombinu wa Halmashauri hiyo Juma Chimwaga amesema kuwa Halmashauri ilipokea shilingi bilioni 8.9 Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo huku miradi kadhaa ikiwa imefikia asilimia 90 ya ujenzi. Amesema kuwa zipo changamoto kama vile ukosefu wa usafiri na na upungufu wa wataalam u wa ujenzi jambo linalopelekea kuchelewa kukamilika Kwa baadhi ya miradi.
Halmashauri nyingine zilizopata nafasi za kuwasilisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi ni pamoja na Halmashauri ya Ifakara Mji, Halmashauri ya Ulanga, Halmashauri ya Kilosa, Halmashauri ya Mlimba, Halmashauri ya Mvomero, Halmashauri ya Gairo na Halmashauri ya Malinyi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa