Wito umetolewa kwa waganga wafawidhi na watoa huduma za afya kiujumla kutambua kazi yao ni wito hivyo wanapaswa kutoa huduma nzuri kwa wananchi wanaowahudumia ili kuepuka malalamiko na kutosababisha laana katika maisha yao na wajikite katika kutoa huduma nzuri ili kuvuna baraka.
Kisena Mabuba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha waganga wafawidhi na watumishi wa afya toka katika Hospitali ya Wilaya , Vituo vya afya na Zahanati ambapo amewataka kutambua kuwa kadri wanavyotoa huduma nzuri ndivyo wanavyosomeka vizuri na kupata baraka.
Mabuba amewakumbusha wahudumu hao kutambua wao ni viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano kwa wengine katika utoaji huduma ambapo amesema kiongozi mzuri ni yule anayeongoza wengine katika njia sahihi huku akisisitiza utendaji kazi unaozingatia kuheshimiana, uaminifu, weledi, ubunifu na bidii katika maeneo yao ya kutolea huduma.
Akizungumzia suala zima la ukusanyaji wa mapato ametaka kila kituo kutoa taarifa zake kila wiki na kusema kuwa zipo huduma ambazo zinatolewa kwa malipo hivyo lazima mapato yakusanywe ili fedha hizo ziweze kusaidia huduma mbalimbali vituoni.
Naye Mganga Mkuu Wilaya Dokta George Kasibante amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwakumbusha mambo muhimu katika sekta ya afya na kusema kuwa utoaji huduma za afya ni huduma muhimu hivyo kila mmoja awajibike katika eneo lake huku akisisitiza suala zima la ukusanyaji wa mapato katika vituo vyao kwa kadri inavyostahiki.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa