Machi 25 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa wajasiriamali wadogo wadogo wasiozidi kipato cha milioni nne kwa mwaka kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vya wajasiriamali wadogo wadogo vitambulisho ambavyo vimetolewa na Mheshimiwa Rais lengo ikiwa ni kuwajali wajasiriamaqli hao ambapo wilaya ya Kilosa mpaka sasa imepokea jumla ya vitambulisho 9500.
Mgoyi ametoa wito huo wakati wa kampeni ya kuhamasisha wajasiriamali hao kuchukua vitambulisho hivyo katika tarafa ya Magole kwa kata za Msoero, Dumila, Mvumi,Magole na Kitete ambapo licha ya kutoa hamasa lakini pia aligawa vitambulisho kwa wajasiriamali wa Dumila na Feri-Magole waliojitokeza kuchukua vitambulisho hivyo vinavyopatikana kwa shilingi 20,000/=.
Akielezea kuhusu vitambulisho hivyo Mgoyi amesema kuwa vinampa fusra mjasiriamali kufanya biashara ya aina yoyote isiyozidi millioni nne kwa mwaka eneo lolote hapa nchini lakini pia kinamsaidia kufanya biashara eneo lolote kwa uhuru huku akiaminika katika maeneo atakayofanyia biashara kupitia uwepo wa kitambulisho hicho.
Aidha amewataka watendaji wa kata, watendaji wa vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji kuongeza kasi ya uhamasishaji na kuwatambua wajasiriamali wanaostahili vitambulisho ili waweze kupatiwa huku akiwasisitiza wafanyabiashara mbalimbali kuwa yapo makundi mawili ambayo ni mfanyabiashara kuwa na namba ya mlipa kodi TIN au kuwa na kitambulisho cha mjasiriamali na kwamba kila mfanyabiashara lazima awe na utambulisho kati ya TIN au kitambulisho na kwa atakayebainika kutokuwa na utambulisho wowote hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Akibainisha aina za biashara na wajasiliamali wanaostahili kupata vitambulisho Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kilosa Reginald Simba amesema wajasiriamli wanaostahili kuwa na vitambulisho ni mama/baba lishe, boda boda, wasusi wa nywele, vinyozi, mafundi viatu, wauza CD na kanda za video, wanaoingiza nyimbo kwenye memory card, wakaanga chips, wauza mbogamboga, waosha magari, wapaka rangi kucha, wauza dawa za mbu na za asili, wakodishaji baiskeli, wauza maji,soda, mafundi seremala, wasukuma maguta/mikokoteni, wauza matunda,mafundi saa au simu, watembeza biashara mikononi na wengine wenye biashara kama hizo.
Licha ya kufanya hamasa katika tarafa ya Magole Mgoyi ametembelea shule za Sekondari Dumila na kujionea ujenzi unaoendelea wakati huo huo diwani wa kata ya Kitete Mh. Steven Lugome akitoa ombi kwa Mkuu wa Wilaya kutembelea shule ya Sekondari Kitete kujionea ujenzi wa madarasa mawili na ofisi unaoendelea na kuwaunga mkono ambapo Mkuu wa Wilaya huyo ametembelea shule hiyo na kutoa ahadi ya kuchangia mifuko 20 ya saruji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa