Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji wilayani Kilosa wametakiwa kutambua vema majukumu yao licha ya uwepo wa ugumu na changamoto mbalimbali zilizopo ambazo haziwaondolei watumishi hao wa umma kufanya majukumu yao ipasavyo kwani wameaminiwa na serikali kuwepo kwa maeneo ya kazi, hivyo wanapaswa kufanya majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za kazi ikiwemo kuwasimamamia kimajukumu watumishi walio chini yao kwa mujibu wa misingi ya utawala bora kwa kuhakikisha wanafanya majukumu yao ipasavyo kwa kuwahudumia wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati wa kikao cha Mkurugenzi huyo kilichoshirikisha Wakuu wa Idara na Vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji ambapo amewataka watumishi hao kusimamia na kukusanya mapato ya Halmashauri kwa kuzingatia uadilifu katika ukusanyaji mapato kwa kusimamia maadili ya utumishi wa umma pamoja na utoaji takwimu sahihi na taarifa muhimu kwa wakati kwa maslahi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
‘‘Aidha niseme kuwa Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji mnao wajibu wa kusimamia miradi ya maendeleo ili ijengwe kwa ubora na ikamilike kwa wakati ili wananchi wapate huduma wanazostahili kwani usimamizi wa miradi ni sehemu ya majukumu yenu ikiwemo utoaji wa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi wa juu kwa kila kinachoendelea hasa katika miradi jambo litakalosaidia Halmashauri kutokuwa na hoja zinazoashiria ubadhirifu wa fedha na maswali ya sintofahamu pindi ziara mbalimbali za viongozi zinapojitokeza pamoja na utoaji huduma bora kwa wananchi bila ya ubaguzi, upendeleo wala viashiria vya rushwa’’. Ameongeza Mwambambale.
Aidha katika kikao hicho Wakuu wa Idara walitoa mada mbalimbali kwa watendaji hao lengo ikiwa ni kuwakumbusha majukumu yao kama watumishi wa umma ambapo miongoni mwa mada hizo ni Uwajibikaji na usimamizi wa mapato, Kuzingatia Dhana ya Utawala bora katika uwajibikaji kwa wananchi, Udhibiti na utatuzi wa migogoro ndani ya jamii na kwa wananchi, Uanzishwaji, utunzaji na uhuishaji wa daftari la wakulima, Kampeni ya ujenzi wa vyoo bora kwa afya bora katika jamii, Uhifadhi na utunzaji wa mazingira na kuepuka athari za uharibifu wa mazingira.
Mada nyingine ni Usimamizi wa vibali vya ujenzi na kuzuia ujenzi holela, Kuanzisha na kuhuisha Rejista za wakazi kwenye vitongoji, Maelekezo na maagizo ya Serikali na Halmashauri, Jumuiya za watumia maji vijijini pamoja na Sheria ndogo, Mikataba na Mabaraza ya kata ambapo mwanasheria wa Halmashauri amewataka watendaji hao kutambua kuwa jukumu la kuandaa mikataba ni la Ofisi ya sheria hivyo linapaswa kuzingatiwa ili kuepuka athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza ikiwemo kukiukwa kwa taratibu na kanuni za mikataba mbalimbali pamoja na kuepuka kesi ambazo zinazoweza kujitokeza dhidi ya Halmashauri.
Katika kuhitimisha kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji amewaagiza watendaji wote kuainisha vyanzo vyote vya mapato katika maeneo yao pamoja na kuainisha uwezo wa kila chanzo sambamba na kufufa akaunti zote za vijiji ili 20% zinazopaswa kurudishwa katika vijiji kwa mujibu wa sheria ziweze kurudishwa kupitia akaunti hizo kwa ajili ya kufanya maendeleo katika vijiji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa