Rai imetolewa kwa wazazi wilayani Kilosa kusimamia na kuutumia ipasavyo waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimumsingi bila malipo ambapo ili kutimiza azma hii serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha kwamba watoto wote wa kitanzania wenye rika lengwa la elimu msingi wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Elimu Wilaya ya Kilosa Nelson Kiliba alipokutana na wazazi, walimu na wajumbe wa kamati za shule mbalimbali wilayani Kilosa ambapo amewataka kuutafuta waraka huo na kuupitia kwa kina ili kutambua yaliyomo ndani yake kisha kuufanyia kazi ipasavyo ikiwemo kutambua majukumu yao kama wazazi/walezi.
’’ Utoaji wa elimumsingi bila malipo una maana ya kwamba mwanafunzi atasoma bila mzazi/mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa ikitozwa shuleni kabla ya kutolewa waraka wa elimu namba 5 wa mwaka 2016 na kwamba Waraka haujasema watoto wasile kwani kula humfanya mtoto ajiamini, asikilize kwa umakini, afikiri vizuri kisha kufaulu vizuri, hivyo mzazi/mlezi anao wajibu wa kuhakikisha anashirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha mtoto wake anakula vizuri awapo shuleni kupitia vikao vitakavyokuwa vimefanya maamuzi kwa kushirikisha wazazi, walimu na kamati za shule. Kiliba amesisitiza
Kiliba amesema kumekuwa na upotoshaji kuhusu waraka huo ambao unamhitaji mzazi kutambua majukumu yake ikiwemo kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia, kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchanai, kukemea na kutoa taarifa ngazi husika kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo na kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya taaluma ya watoto wao
Akizungumzia kuhusu suala la wanafunzi wasiochangia kuzuiwa kula Kiliba amesema walimu wasiwazuie wanafunzi bali wazazi wote watakaokaidi maamuzi ya kikao ya uchangiaji wa chakula wachukuliwe hatua stahiki ili kukomesha tabia hiyo na kuondoa malalamiko baina ya wazazi na uongozi wa shule.
Sambamba na hayo wazazi waliohudhuria vikao hivyo wamemshukuru Afisa Elimu Wilaya kwa kuwaelimisha juu ya waraka huo na wameahidi kusimamia vema na kushiriki kikamilifu katika masuala ya kielimu ili kusonga mbele na kuwa bega kwa bega na walimu ili kupata matokeo chanya ikiwemo ufaulu mzuri kwa wanafunzi hasa wa darasa la nne na la saba.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa