Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa wajumbe wa bodi ya afya Wilaya kuzingatia wajibu na majukumu yao katika kuboresha huduma za afya na kutenda haki kwa kila mtu na kutoa maamuzi sahihi kwa muda sahihi ili mwisho wa siku tuungane pamoja na serikali katika kuboresha huduma za afya na kwamba ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, itaendelea kutoa ushirikiano kwa kufanya kazi kwa karibu na bodi.
Mgoyi amesema hayo wakati wa uzinduzi wa bodi ya afya Wilaya ambapo amesema kuwa Bodi na Kamati za vituo vya kutolea huduma za afya zipo kwa mujibu wa sheria na zina majukumu mbalimbali ya kutekeleza ikiwa ni pamoja na kujadili na kurekebisha mipango ya Afya na Bajeti na kuziwasilisha Halmashauri ili iidhinishwe.
Aidha amesema bodi inao wajibu wa kupokea, kuchambua na kuidhinisha taarifa za Utekelezaji shughuli za idara kutoka kwa timu ya Uendeshaji wa huduma za Afya ya Halmashauri (CHMT),kubuni na kushauri vyanzo mbalimbali vya mapato, na pia ameitaka bodi hiyo kushirikiana na Kamati za Afya na Washirika wengine kwa kuinua kiwango cha utoaji huduma ya Afya na kuwa na uhusiano wa kiutendaji na kamati za usimamizi za Vituo na kwamba haitangilia mambo ya kitaalamu ya Watumishi katika maadili ya kikazi.
Pia ameitaka bodi hiyo kuwa chachu ya ufanisi ya kuhakikisha huduma za afya ziko vizuri na pindi zinapopata malalamiko zisiamini kabla ya kuona hivyo pindi zinapopokea malalamiko zifanye ufuatiliaji ili kubaini ukweli wa jambo husika pamoja kusimamia uboreshwaji huduma za afya katika vituo vya afya sambamba na kuongeza kasi ya uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya CHF kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupata ongezeko la mgawanyo wa dawa katika Wilaya.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Dkt. Fred Mwanyesya amesema kuwa kila mmoja awajibike kwa nafasi yake na kutofanya kazi kwa mazoea ili kuleta mabadiliko katika Wilaya ya Kilosa na ameahidi wao kama bodi wataendeleza mabadiliko yaliyopo ikiwemo kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF lakini pia kusaidia kuongeza na kusimamia vyanzo vingine vya mapato ikiwemo kusimamia rasilimali za vituo vya afya na kutilia mkazo upatikanaji wa watumishi wa afya sambamba kutofanyia kazi majungu bali iko tayari kufanyia kazi mambo yaliyo na ukweli.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa